NA FRED KIBANO
SERIKALI imepongeza kasi ya ujenzi wa madarasa kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza 2022 yanayoendelea kujengwa mkoani Lindi licha ya kuwa katika hatua tofauti tofauti za ujenzi.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt.Festo Dugange ametoa pongezi hizo alipofanya ziara yake ya kikazi Novemba 26, 2021 wilayani Kilwa mkoani Lindi ambapo amejionea kasi ya ujenzi na uwepo wa vifaa vyote muhimu kwa hatua zote zilizobaki na kwamba dhamira ya Serikali ya kuamua kutokuwa na machaguo zaidi ya mawili mwaka 2022 itafikiwa.
Dkt. Dugange amesema,Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa pekee imepokea kiasi cha shilingi Bilioni moja na milioni mia sita kwa ajili ya kujenga madarasa 74 ya sekondari na madrarasa 29 ya shule shuikizi ambayo yote yatatumika katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari, 2022.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha watoto wetu wote ifikapo Januari 2022 wanaingia darasani siku moja, bila kuwa na chaguo la kwanza, chaguo la pili na chaguo la tatu ambapo mara nyingi yale machaguo yalikuwa yanachangiwa na uhaba wa madarasa au ufinyu wa madarasa, tulikuwa na utaratibu wa kujenga madarasa kwa zimamoto muda wa watoto kuingia darasani unafika madarasa hayajakamilika.
"Ndio maana Serikali sasa imedhamiria kuhakikisha inapofika tarehe ya kufungua shule kidato cha kwanza watoto wetu wote wa sekondari wanaaza siku moja masomo yao ya kidato cha kwanza,” amesema Dkt. Dugange.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Bw. Shaibu Ndemanga amesema, wadau wote muhimu wameshirikishwa wakiwemo Madiwani, Wakuu wa shule, watendaji wa kata na menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya na matarajio kuwa ujenzi wa madarasa utakamilika mapema tarehe 15 Desemaba, 2022.
Dkt.Dugange amesema, utekelezaji wa ujenzi huo utaweza kufikia malengo ya Serikali endapo tarehe iliyowekwa kitaifa ya kukamilisha ujenzi itazingatiwa na halmashauri zote ambayo ni tarehe 15 Desemba mwaka huu kwa kuongeza kasi zaidi na hata kujenga usiku na mchana.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Kilwa, Jason Kashaija amesema, shule yake ilipokea kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya na watarajia kumaliza ujenzi mapema ifikapo tarehe 15 Desemba na kwamba vifaa vyote vinavyohitajika kwa hatua za umaliziaji vyote vimekwisha nunuliwa
Aidha, Kashaija amesema ujenzi mapaka sasa umegharimu shilingi milioni 24,611,000 na kati ya fedha hizo milioni 2,800,000 zimetumika kuwalipa mafundi lakini pia wanakabiliwa na changamoto za wananchi kutokuwa tayari kujitolea nguvu zao baada ya kusikia Serikali imetoa fedha kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa madarasa ya shule hiyo pamoja na bei ya vifaa vya ujenzi kuwa ghali wilayani Kilwa na hivyo kupelekea kuagiza vifaa vya ujenzi kutoka nje ya wilaya hiyo.