NA JAMES K.MWANAMYOTO,Arusha
Serikali imesisitiza kutowarejesha kwenye Utumishi wa Umma watumishi 15,538 walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti au kutoa taarifa za uongo katika kumbukumbu zao rasmi za kiutumishi kuwa wana elimu ya kidato cha nne.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Arusha kuhusu msimamo wa Serikali wa kutowarejesha watumishi wa umma walioghushi vyeti vya elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita na ualimu (Stashada na Daraja A). Kulia kwake ni Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Mohamed Mchengerwa amesema, msimamo wa Serikali wa kutowarejesha
watumishi hao waliobainika kughushi vyeti uko palepale.
“Ninasisitiza
kuwa, hakuna msamaha wowote uliotolewa na Serikali kuwarejesha
watumishi waliokosa uadilifu kwa kughushi vyeti au kutoa taarifa za
kiutumishi zisizo sahihi,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Aidha,
Mhe. Mchengerwa ameuarifu umma kuwa, Serikali imewaondoa pia watumishi
hewa 19,708, hivyo kuiwezesha Serikali kuokoa kiasi cha shilingi bilioni
19 ambazo zinatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akizungumzia
watumishi waliorejeshwa kazini baada ya kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara, Mhe. Mchengerwa amesema, mwaka 2004 Serikali ilitoa
Waraka uliobainisha kwamba watumishi wote watakaoajiriwa kuanzia tarehe
20 Mei, 2004 walitakiwa kuwa na elimu ya Kidato cha Nne ikiwa ni
utekelezaji wa matakwa ya Sera ya Ajira na Menejimenti ya Utumishi wa
Umma pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akizungumza nao leo jijini Arusha kuhusu msimamo wa Serikali wa kutowarejesha Watumishi wa Umma walioghushi vyeti vya elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita na ualimu (Stashada na Daraja A).
Mhe. Mchengerwa
ameongeza kuwa, katika utekelezaji wa matakwa hayo, mwaka 2017 wakati wa
zoezi la uhakiki wa vyeti na watumishi hewa ilibainika baadhi ya
watumishi wenye elimu ya Darasa la Saba waliajiriwa bila kuwa na
cheti cha ufaulu wa elimu ya Kidato cha Nne. Hivyo, watumishi hao waliondolewa kazini kutokana na kukosa sifa kwa mujibu wa Miundo ya
Utumishi ya Kada zao.
Amesema katika zoezi hilo, baadhi ya waajiri waliwaondoa kwenye Orodha ya Malipo ya Mishahara kimakosa
watumishi wasiokuwa na elimu ya Kidato cha Nne walioajiriwa kabla ya
tarehe 20 Mei, 2004. Kutokana na makosa hayo, mwaka 2018 Serikali
kupitia Waajiri na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora iliwarejesha kazini na kuendelea kuwalipa mishahara jumla
ya watumishi 4,380 walioondolewa kwenye Orodha ya Malipo ya Mishahara
kimakosa. Idadi hii inajumuisha Watendaji wa Kata, Watendaji wa Mtaa na
Watendaji wa Kijiji wapatao 3,114.
Pamoja na kuwarejesha
watumishi tajwa, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali pia ilitoa msamaha wa
kuwarejesha kazini watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya
elimu ya Kidato cha Nne na baadaye wakajiendeleza na kupata sifa tajwa
hadi kufikia mwezi Desemba, 2020.
Msamaha huu uliwahusu watumishi
waliojipatia vyeti vya elimu ya Kidato cha Nne ambao hawakudanganya
katika taarifa zao kuwa wana elimu ya Kidato cha Nne au hawakubainika
kughushi vyeti.
Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha
Mhe. Mchengerwa kuzungumza na Waandishi wa Habari, Katibu
Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema lengo la Mhe. Mchengerwa
kuzungumza na Vyombo vya Habari ni kutoa ufafanuzi juu ya upotoshwaji
unaofanywa na baadhi ya mitandao ya kijamii kuwa Serikali imeamua
kuwarejesha kazini watumishi walioghushi vyeti na walioajiriwa kwa cheti
cha darasa la saba ambao walishindwa kujiendeleza ili kupata sifa
stahiki hadi kufikia mwezi Desemba, 2020 kama Serikali ilivyoelekeza.
Katibu Mkuu-UTUMISHI, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Arusha kuhusu msimamo wa Serikali wa kutowarejesha Watumishi wa Umma walioghushi vyeti vya elimu ya kidato cha nne, kidato cha sita na ualimu (Stashada na Daraja A).
Ameongeza
kuwa, Ofisi yake iliwaandikia waajiri wote barua tarehe 7 Mei, 2021
kuelekeza namna ya kuhitimisha suala la hilo ambalo waathirika wamekuwa
wakiibua hoja nyingi ambazo tayari Serikali ilishazitolea maamuzi.
Dkt.
Ndumbaro amesema upotoshwaji unaendelea kufanywa licha ya Mhe. Waziri
Mkuu, Msemaji wa Serikali na Mhe. Mchengerwa mwenyewe kutoa ufafanuzi wa
suala hili hivi karibuni, hivyo Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa
Umma ameona ni vema akazungumza tena na Vyombo vya Habari ili kulielezea
kwa kina suala hili na hatimaye jamii ielewe hatua zilizochukuliwa na
Serikali na msimamo wake.
Tags
Habari