Serikali yawaonyesha vijana ilipo fursa ya kujikwamua kiuchumi

NA MWANDISHI MAALUM

VIJANA wameaswa kuthamini na kutumia ipasavyo fursa ya mafunzo ya ufundi stadi yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu maana ni suluhisho la kuzalisha wataalamu mahiri wenye ujuzi na stadi zinazohitajika katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi akiangalia mfumo wa umeme wa majumbani na viwandani alipotembelea na kukagua mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa Uanagenzi wakati wa mahafali hayo ya 22 ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help yaliyofanyika Jijini Arusha, Novemba 19, 2021. Kulia ni Joyce Mayala mnufaika wa mafunzo hayo ya Uanagenzi.

Ameyasema hayo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi aliposhiriki katika mahafali ya 22 ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help kilichopo Mtaa wa Sakina, Arusha Novemba 19, 2021.

Naibu Waziri Katambi alieleza kuwa, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo inalenga kuimarisha nguvukazi iliyo katika soko la ajira kwa kuipatia ujuzi na stadi za kazi.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu imeendelea kuwatengenezea vijana mifumo maalumu ya kupata ujuzi ili waweze kuondokana na changamoto ya ajira kwa kuwapatia mafunzo yenye ujuzi staki unaohitajika katika soko la ajira,” alisema Naibu Waziri Katambi.
Mnufaika wa mafunzo ya Uanagenzi Monica Damiani (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kutoka kulia) alipotembelea fani ya ushonaji katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help.

Alifafanua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu iliingia makubaliano na Vyuo 72 ambavyo vinatoa mafunzo ya ufundi stadi na jumla ya vijana 14,440 katika mikoa yote ya Tanzania bara wamenufaika na programu hiyo kwa kulipiwa ad ana serikali asilimia 100.

“Mafanikio tunayoyaona katika utekelezaji wa programu hii yanatupa hamasa ya kuendelea kutoa fursa zaidi ya mafunzo haya ili kuwezesha nguvukazi ambayo asilimia kubwa ni vijana kujiajiri na kujikwamua kiuchumi,” alisema.

Alieleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa na mchango mkubwa kwa vijana hususan katika kuongezeka kwa fursa za ajira na uwezo wa kuajirika pamoja na baadhi yao wamepata ajira kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

“Ukienda kwenye mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji – Julius Nyerere, mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta asilimia kubwa ya vijana walioajiriwa ni wanufaika wa mafunzo haya ya uanagenzi,” alisema.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (wa pili kutoka kushoto) akigawa cheti kwa mwanafunzi bora wa mafunzo ya Uanagenzi Bw. Frank Kijangwa (kulia) katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help wakati wa hafla hiyo.

Aidha, Naibu Waziri Katambi ametaka vijana wanaohitimu mafunzo hayo kutumia maarifa na ujuzi wao kujiajiri na kujikwamua kiuchumi ili kuondokana na umaskini.

Sambamba na hayo amezitaka Halmashauri zote nchini kuwa na kanzi data ya vijana wanaopatiwa mafunzo ya ufundi stadi katika meneo yao ili kuwawezesha mikopo ya asilimia 4 kupitia mapato ya ndani.

“Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alielekeza wakati wa uzinduzi wa programu hii ya awamu ya tatu kule Jijini Mbeya vijana hawa waliosomeshwa kwa ufadhili wa serikali wapatiwe mikopo hiyo ili waweze kuanzisha miradi au shughuli mbalimbali za kiuchumi zitakazo wawezesha kujiajiri, kuajiri wenzao na kujiingizia kipato,” alisema Katambi

Pamoja na hayo alitumia fursa hiyo kuwapongeza vijana hao waliohitimu mafunzo hayo na aliwasihi kuwa mfano wa kuigwa katika utendaji wa kazi zao kwenye jamii zinazowazunguka kwa kuonyesha uwezo wao katika kumudu kazi.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo hicho cha Ufundi Stadi cha Help to Self Help na baadhi ya wanafunzi waliohitimu mafunzo ya uanagenzi katika fani mbalimbali. (Picha na OWM).

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Help to Self Help Bw. Amani Sam alitumia fursa hiyo kuishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuwapatia nafasi ya kutoa mafunzo ya uanagenzi.

“Tunaishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kutekeleza mpango huu wa kuwapatia vijana ujuzi katika fani mbalimbali na jumla ya Vijana wapatao 150 wamepatia mafunzo ya uanagenzi toka mwezi juni 2021,” alisema

Mnufaika wa Mafunzo hayo Bi. Dina Lukasi ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali na kutambua mchango wa vijana katika jamii kwa kuwapatia ujuzi ambao utakuwa na manufaa katika kuwawezesha kuondokana na changamoto ya ajira.

“Tunamshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake kwa kutupatia fursa hii, hakika mafunzo tuyopata yamekuwa na faida mno kwetu,” alisema Mwanagenzi huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news