'Spider Track' yashindwa kuonyesha ilipo ndege na rubani aliyepotea Tunduru

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Baada ya DIRAMAKINI BLOG kuripoti hivi karibuni kuhusu kupotea kwa ndege ndogo yenye usajili 5H-WXO aina ya BatHawak na rubani wake wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea na juhudi za kuitafuta.
Juhudi hizo zinaendelea zikiwa ni zaidi ya siku 10 zimepita sasa ambapo,kifaa aina ya 'Spider Track' ambacho kina uwezo wa kuonesha ndege hiyo inayomilikiwa na shirika lisilo la kiserikali la Protected Areas Management Solution Foundation (PAMS) bado hakijaonesha ndege hiyo wapi ilipita.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mheshimiwa Julias Mtatiro amesema kuwa, ndege hiyo aina ya BatHawak inayorushwa na rubani Samwel Balina Gibuy imepotea Oktoba 18, mwaka huu majira ya saa 9.:09 jioni ikiwa inaelekea Kingupira katika Pori la Akiba la Selous.Soma hapa, rubani apotea na ndege ndogo>>>

Amesema kuwa, ndege hiyo iliombwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kupitia Shirika la Uhifadhi la Frankfurt Zoologocal Society (FZS) kwa lengo la kwenda kusaidia katika zoezi linaloendelea la utafutaji wa faru weusi katika pori la akiba la Selous.

"Muda mfupi baada ya kuruka ndege ilionekana na wachimbaji wa madini eneo la Matuli na baadae wananchi wa Kijiji cha Kajima kilichopo katika Kata ya Jakika Tarafa ya Matemanga wilayani Tunduru ikielekea uelekeo wa Mashariki mwa Kijiji cha Kajima ambacho kinakadiriwa kuwa na umbali wa kilomita 26 kutoka uwanja wa ndege wa Matemanga ambapo ndege hiyo iliruka wakati wa kuondoka," amesema Mkuu huyo.

Amesema, ndege hiyo ilitarajiwa kutuwa Kingupira majira ya saa 11:30 hadi 12:09 jioni ambapo kwa bahati mbaya haikufika Kingupira kama ilivyotarajiwa na ndipo mawasiliano ya kuulizia kwa pande zote mbili ilikotoka na inako kwenda yalianza.

Mheshimiwa Mtatiro amesema kuwa, baada ya kujiridhisha kuwa ndege hiyo haikufika Kingupira na wala haijaonekana kwenye uwanja wa ndege wa Matemanga ambapo ndiko kuna ofisi za PAMS Foundation wafanyakazi wenzake rubani Samwel walimjulisha Mkurugenzi wa shirika hilo.

Amesema, baada ya kufahamishwa aliangalia kwenye 'Spider Track' ya ndege hiyo yenye uwezo wa kuonesha alikopita na ilipo ndege hiyo na kwamba Spider track ilionesha kuwa ndege hiyo ilikuwa uwanjani majira ya saa 7 mchana ambapo muda huo alikuwa anafanya majaribio kabla ya safari kuanza na baada ya kuruka akielekea Kingupira Pori la Akiba la Selous spider track haikuonesha chochote.

Amesema kuwa, taarifa zilitolewa katika ngazi za mamlaka mbalimbali huku maandalizi ya utafutaji na uokozi yikiendelea ambapo kazi hiyo imefanyika kwa siku kadhaa kwa kutumia jumla ya ndege tano.

Amesema, kati ya ndege hizo nne za mabawa na moja ni helikopta na wameamua kuimarisha zoezi hilo na kuwaomba wananchi na vyanzo vingine kuendelea kutafuta ndege hiyo na kwamba zawadi nono itatolewa kwa yeyote atakayefanikiwa kutoa taarifa ya ndege hiyo.

Kaka wa rubani huyo,Jani Killa akizungumza kwa niaba ya familia amesema kuwa, wamepokea kwa masikitiko makubwa sana kupotea kwa ndugu yao, lakini kwa kushirikiana na shirika la PAMS na Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama wanahakikisha wanampata ndugu yao, lakini pia kupatikana na ndege aliyokuwa anaitumia.

Mratibu wa mradi wa uhifadhi wa Tembo Ruvuma kwenye Shirika la PAMS Foundation, Osca Bakumbezi amesema kuwa, tukio hilo ni la simanzi kwa sababu kwanza rubani wao walikuwa wanafanya nae kazi muda wote na wameshirikiana nae kwenye kazi nyingi.

Amesema kwamba, hata kazi aliyokuwa anaenda kuifanya ni kazi ambayo ilikuwa na manufaa makubwa kwa Taifa na si vinginevyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news