TAKUKURU ni tegemeo kubwa la Serikali katika kudhibiti ubadhirifu, rushwa-Ndejembi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi amesisitiza kuwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) ni tegemeo kubwa kwa Taifa hususani katikali kudhibiti ubadhirifu na vitendo vya rushwa nchini.
"Nami napenda nitumie fursa hii kusisitiza kuwa taasisi yenu ndiyo tegemeo la Serikali katika kudhibiti ubadhirifu na vitendo vya rushwa, mambo ambayo ni moja ya vikwazo vikuu vinavyokwamisha maendeleo ya Taifa letu.

"Hivyo, ni lazima tushirikiane katika kuwajenga viongozi wazalendo, wenye kufuata sheria, kanuni na misingi ya utawala bora katika kutekeleza majukumu yao;

Mheshimiwa Ndejembi ameyasema hayo leo Novemba 27, 2021 wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka 2021 wa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) uliofanyika kuanzia Novemba 25 hadi leo jijini Dodoma.

Mkutano huo uliwakutanisha pamoja Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salum Rashid Hamduni,Bibi Neema Mwakalyelye ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Wakurugenzi wa TAKUKURU, Wakurugenzi Wasaidizi, Wakuu wa Vitengo, Wakuu wa TAKUKURU Mikoa 28 na watumishi wengine wa TAKUKURU

"Kipekee kabisa ninaomba kutumia fursa hii kuwapongeza sana kwa utaratibu huu wa viongozi waandamizi wa TAKUKURU kukutana kila mwaka kwa lengo la kutathmini utendaji kazi wa majukumu mliyotekeleza kwa kipindi cha mwaka uliopita na kuainisha changamoto zilizojitokeza katika kipindi husika pamoja na kujadili na kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo kwa lengo la kuboresha utendaji kazi kwa kipindi cha mwaka 2021/2022. Hongereni sana.

"Kwa uzoefu wangu, nikiri wazi kuwa ni taasisi chache sana ambazo zinatambua umuhimu wa kufanya tathimini ya utendaji kazi wao kupitia mikutano ya viongozi wa taasisi husika. Utaratibu huu wa kufanya mikutano na kufanya tathmini ya utendaji kazi na kupanga namna bora ya kuboresha utendaji kazi ni muhimu sana hususani kwa taasisi ambayo ina nia ya kufikia malengo yake.

"Kwa kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametupa dhamana hii adhimu ya kusimamia Utawala Bora nchini pamoja na mapambano dhidi ya rushwa, ninawasihi tusimame imara kweli kweli katika majukumu haya adhimu kwa mustakabali wa Taifa letu,"amefafua Mheshimiwa Ndegembi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kufunga mkutano huo.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa, tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, amekuwa akifuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU ambayo ni uelimishaji, uzuiaji rushwa, uchunguzi na uendeshaji wa Mashtaka. "Kwa kweli mnastahili pongezi. Hongereni sana.

"Pamoja na ufanisi katika utendaji kazi wenu, bado kuna kila sababu ya kuendelea kuwadhibiti watumishi wenu wanaofanya kazi kwa mazoea na wanaojihusha na ukiukwaji wa maadili kabla hawajachafua taswira chanya ya chombo hiki nyeti kwa Taifa letu.

"Ni jambo la kujivunia kwamba mwitikio wa viongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita katika mapambano dhidi ya rushwa ni mkubwa na ndiyo maana wengi wao wamekuwa wakisikika kila kona wakikemea uvunjifu wa maadili ikiwemo kujihusisha katika vitendo vya rushwa.

"Ninyi ni mashahidi wa hiki ninachokisema kwa kuwa, viongozi wengi wamekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa maelekezo yanayohusu ushughulikiaji wa vitendo vya
rushwa moja kwa moja kwenu,"ameongeza Mheshimiwa Ndejembi.

Pia amesema kuwa, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine barani Afrika na Duniani kwa ujumla, inakabiliwa na tatizo la uwepo wa rushwa na mmomonyoko wa maadili.

Amesema, vitendo hivi vinachangia sana kuzorotesha maendeleo ya nchi pamoja na ukuaji wa uchumi. "Ni rai yangu kuwa wakati mnaondoka kurudi katika vituo vyenu vya kazi muanze kupanga mikakati wa kukabiliana au kupunguza changamoto hizi.

"Sote tunafahamu adhma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kutaka kuendelea kuleta maendeleo katika Taifa letu, hivyo ni jukumu lenu kama taasisi iliyopewa dhamana na Serikali kuhakikisha vitendo vya rushwa vinadhibitiwa katika sekta zote na hasa zile zilizopewa kipaumbele katika Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na Rushwa na Mpango Mkakati ambao unatekelezwa kwa Awamu ya Tatu (National Anti-Corruption Strategy and Action Plan –
NACSAP III),"amesema.

Mheshimiwa Naibu Waziri huyo amesema kuwa, sekta hizo ni pamoja na manunuzi ya umma, ukusanyaji wa mapato, utoaji wa haki, maliasili na utalii, madini, nishati, mafuta na gesi, afya, elimu na ardhi.

Amesem,sekta hizi zote ukiziangalia ni muhimu katika kufanikisha ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini, hivyo anawasihi mipango na mikakati yao ilenge kuzuia zaidi ili kuisaidia Serikali kufikia malengo yake.

"Kama mnavyofahamu mapambano dhidi ya rushwa si ya TAKUKURU peke yake hivyo basi muendeleze ushirikiano na vyombo vingine vya Kitaifa na Kimataifa.

"Ninafurahishwa sana ninavyoona ushirikiano mkubwa ambao mnao na na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, PPRA, TRA, Mahakama ya Tanzania, Asasi za Kiraia pamoja na wadau wengine. Ushirikiano
huu ni jambo muhimu sana ambalo linasaidia utekelezaji wa majukumu yenu kuwa rahisi na yanayotekelezeka kwa wakati.

"Ninafahamu pia kwamba bado mnaendelea kushirikiana na Taasisi Simamizi za Sekretariati ya Maadili, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora pamoja na Taasisi nyingine ambapo mwezi ujao mtaadhimisha kwa pamoja SIKU YA MAADILI NA HAKI ZA BINADAMU. Hili ni jambo jema sana kwa sababu mapambano dhidi ya rushwa hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano kutoka kwa wadau wa pande zote.

"Wakati Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa - Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mejimenti ya Utumishi na Utawala Bora alipokuwa anafungua Mkutano huu wa viongozi, pamoja na mambo mengine alieleza historia ya mapambano dhidi ya rushwa nchini, lakini pia alieleza kwamba kuundwa kwa taasisi hii ilikuwa ni azma ya Serikali ya kujenga nguzo kuu za Serikali za kuongeza ufanisi na uwajibikaji wa umma, wenye miiko ya maadili na kuwa na jamii isiyojihusisha na vitendo vya rushwa,"ameongeza.

Mheshimiwa Ndegembi amesema kuwa, njia pekee itakayotuwezesha kufanikisha azma hii ni kuendelea kutoa elimu kwa viongozi na wananchi kwa ujumla juu ya athari za rushwa na kufuata maadili mema.

"Aidha, endeleeni kushirikiana na na Kitengo cha Maboresho na Utawala Bora – Ofisi ya Rais IKULU katika kusimamia utekelezaji wa NACSAP III kwa sababu Mkakati huu umebeba ajenda ya Rushwa na TAKUKURU ndicho chombo chenye dhamana ya kusimamia mapambano dhidi ya rushwa kisheria.

"Kwa upande wetu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tumedhamiria kuendelea kusimamia Sera zilizopo katika kuhakikisha kwamba viongozi wanatekeleza majukumu yao katika misingi ya utawala bora.

"Pia nimejulishwa kuwa kwa kipindi cha siku tatu za Mkutano Mkuu mada mbali mbali zimejadiliwa zikiwemo za ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, Usimamizi wa Uchunguzi wa Makosa ya Rushwa,

"Misingi ya Maadili, Mwongozo wa Namna ya Kushudhulikia Mashauri ya Kinidhamu, Namna ya kudhibiti hisia hasi (emotional intelligence) pamoja na Mahusiano kazini. Ninaamini mada hizi zikitumika vizuri zitaboresha utendaji kazi wenu na kuboresha maaadili na mahusiano kati yenu na watumishi walioko chini yenu.

"Nimesikia katika hotuba ya Mkurugenzi Mkuu kuhusu Maazimio mliyoyapitisha katika Mkutano Mkuu huu, kwa kweli maazimio haya yanalenga kuboresha utendaji kazi wenu na kuondoa utendaji kazi wa mazoea, ninawasihi mkayatekeleze maazimio yote kama mlivyokubaliana.

"Aidha, msipotekeleza maazimio hayo yote mtaondoa maana nzima ya kuitishwa kwa mkutano huu. Ninawatakia utekelezaji mwema wa maazimio mliyoyafikia pamoja na mikakati mliyojiwekea katika mkutano huu,"amebainisha Naibu Waziri Ndejembi.
Novemba 25, 2021 wakati akifungua mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anaamini kuwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) itamsaidia kujenga taifa ambalo wananchi anaowaongoza watanufaika na uwepo wa rasilimaliwatu na rasilimali za umma zilizopo pasipo kuombwa wala kutoa rushwa.

Mhe. Mchengerwa amesema, mapambano dhidi ya rushwa yamejikita katika misingi ya Utawala Bora, hivyo amewataka viongozi wa TAKUKURU kujipanga katika mapambano dhidi ya rushwa ili taifa liwe na watumishi na taasisi za umma zinazotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya Utawala Bora.

Ameongeza kuwa, moja ya vinyemelea vya rushwa katika Taasisi za Umma ni urasimu wa utoaji wa huduma hivyo kama utoaji wa huduma utazingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo hakuna mwananchi atakayeshawishika kutoa rushwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu kutoka katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Salumu Hamduni amesema wametekeleza majukumu na kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021 jumla ya shilingi bilioni 29.3 ziliokolewa ambapo bilioni 11 .2 ziliokolewa kwa mfumo wa fedha taslimu na utaifishaji mali na kiasi cha bilioni 18 zilidhibitiwa kabla hazijatumika.
Amesema, miradi ya kimaendeleo 1,188 zenye thamani ya bilioni 714.17 katika sekta ya afya, maji, elimu ziliweza kufatiliwa na kuona makosa ambayo wameyachukulia hatua.

“Tumeelimisha katika ngazi ya makao makuu pamoja na wakuu wa TAKUKURU kuzuia vitendo vya rushwa kuelimisha, kushirikisha jamii pamoja na kuwafikisha watumiwa mahakamani kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka majalada 1,053 yalichunguzwa na kukamilishwa na majadala 339 yaliwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kuomba kibali cha kuwafikisha mahakamani ambapo kesi mpya zilipatikana 542, na kesi 541 zilitolewa uamuzi ambapo Jamhuri iliweza kushinda kesi 345,”amesema Hamduni

Aidha, akizungumzia changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, Hamduni amesema ni pamoja na ufinyu wa bajeti ambao umeathiri uchunguzi, mafunzo kwa wafanyakazi, ununuzi wa vifaa na mahitaji mbalimbali pamoja na uhaba wa wafanyakazi.

Aidha, akizungumzia changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, Hamduni amesema ni pamoja na ufinyu wa bajeti ambao umeathiri uchunguzi, mafunzo kwa wafanyakazi, ununuzi wa vifaa na mahitaji mbalimbali pamoja na uhaba wa wafanyakazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news