NA DOREEN ALOYCE
TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa maonesho ya kihistoria ya Juakali na Nguvukazi ya Afrika Mashariki (EAC) huku yakishirikisha wajasiriamali takribani 1,000 ambapo yatafanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza na yataenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 Uhuru.
Akizungumza jijini hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amesema maonesho hayo ya Afrika Mashariki yatafanyika kati ya Desemba 2 hadi 12, mwaka huu.
Mhagama amesema, pamoja na maonesho pia kutakuwa na makongamano ambayo mada mbalimbali zitatolewa zikiwemo za namna ya kupata mitaji, masoko, ubora wa bidhaa, urasimishaji bidhaa na uongezaji thamani wa bidhaa za washiriki hasa wajasiriamali, vijana na wenye ulemavu.
Amesema kuwa, Maonesho hayo ni ya sita kuandaliwa na Tanzania na yalifanyika kwa mara ya kwanza Desemba 1999 jijini Arusha, wakati Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ilipozaliwa upya ambapo viongozi wa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda walikubaliana yawe yanafanyika kwa mzunguko kutoka nchi moja hadi nyingine.
Katika mzunguko huo, Tanzania imekuwa mwenyeji wa maonesho hayo mara tano na hii itakuwa ya sita. Pamoja na ya mwaka 1999, pia iliandaa ya mwaka 2003, 2006, 2009,na 2015 ambayo yote yalifanyika jijini Dar es Salaam na ya mwaka huu ambayo yatakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru uliopatikana Desemba 9, 1961 yanafanyika jijini Mwanza.
Mhagama amesema katika maonesho hayo, Tanzania ikiwe mwenyeji itakuwa na wajasiriamali 450, hivyo akawahimiza wale wote wanaotaka kushiriki kupata fomu za kujiunga kwa wakurugenzi wa halmashauri, miji, majiji na kwenye tovuti ya ofisi ya waziri mkuu.
"Kwa kutambua umuhimu wa maonesho haya tunategemea kuwa na zaidi ya Wajasiriamali 1,000 kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Tanzania ambao watashiriki katika maonesho haya ambapo Tanzania itawakilishwa na Wajasiriamali zaidi ya 450,"amesema.
"Kwa wajasiriamali, vijana na wenye ulemavu wanatakiwa kutumia fursa ya maonesho hayo ya nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda, Sudani Kusini, Burundi, Rwanda na Tanzania kama wenyeji wanatakiwa kuyatumika katika kutangaza kazi, bidhaa na ubunifu wao kwenye teknolojia ya habari, viwanda biashara na huduma za jamii."amesema Mhagama.
Aidha amesema wajasiriamali wenyeji wanatakiwa kuyatumia kama kipimo cha ubora wa bidhaa zao wakilijilinganisha na wenzao namna gani bidhaa zao zitatumia fursa hiyo kutafuta masoko ndani ya nchi na katika ukanda huo na ndio fursa kwao kurasimisha huduma na bidhaa zao.
Pia ameongeza kwamba wajasiriamali wanatakiwa kutumia maonesho hayo kama chachu ya kuboresha bidhaa na huduma zao mara baada ya kujifunza na kuiga teknolojia, ujuzi na ufundi kutoka nchi wanachama.
Mhagama amesema, maonesho ya mwaka huu kaulimbiu yake ni: "Kuhimiza Ubora, uvumbuzi ili kuunganisha wajasiriamali wadogo na wa kati wa Afrika Mashariki ili kuwainua kiuchumi hasa kutokana na janga la Covid-19."
Maonesho ya mwaka huu kutokana na umuhimu wake, timu maalumu imeundwa ikishirikisha watendaji wa ofisi ya waziri mkuu kama mratibu wa wajasiriamali, vijana na wenye ulemevu pia masuala ya uwezeshaji kiuchumi, pia maofisa kutoka Zanzibar, ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza na Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Tanzania.
Mhagama ametoa wito kwa wadau wote kuandaa wajasiliamali wakiwemo Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) kuwaibua vijana wafanyabiashara wadogo na wa kati kutumia fursa hiyo na kwenda kwa wakurugenzi kupata fomu za kujisajiri ili kushiriki maonesho hayo.