NA MWANDISHI MAALUM
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati zikiwemo nishati, utalii, usafirishaji, viwanda, kilimo na uvuvi kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimtambulisha mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni kwa wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni yaliyofanyika leo tarehe 27 Novemba 2021, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa ya mazungumzo baina yao kwa waandishi wa habari, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania na Uganda zimeendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ya uwekezaji na biashara kwa miaka mingi ambapo hadi sasa Uganda ni nchi ya pili kwa uwekezaji nchini Tanzania kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tumezungumza masuala mengi na Mhe. Rais Museveni na tumekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo kati yetu hususan kwenye sekta za manufaa kwetu sote. Pia tumekubaliana kuimarisha biashara na uwekezaji baina yetu na ninafurahi kuwajulisha kuwa hadi sasa Uganda ni nchi ya pili kwa uwekezaji nchini Tanzania kwa ukanda wa Afrika Mashariki ambapo ipo miradi 45 yenye thamani ya Dola milioni 114 na imewezesha kutoa ajira kwa watanzania 2150”, amesema Mhe. Samia.
Kuhusu masuala ya biashara, Mhe. Rais Samia amesema mwenendo wa biashara kati ya Tanzania na Uganda ni mzuri ambapo hadi kufikia mwaka 2020 ujazo wa baishara kati ya nchi hizo umeongezeka hadi kufikia Shilingi bilioni 607 kutoka shilingi bilioni 200 mwaka 20214.
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akisalimiana na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala. Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb), Balozi wa Tanzania Nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima pamoja na Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Aziz.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni Ikulu Jijini Dar es Salaam
Kadhalika, viongozii hao wamewaagiza Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya biashara wa Tanzania na Uganda kukutana mara kwa mara ili kutatua changamoto mbalimbali za ufanyaji biashara na kuwataka kukutana katika kipindi cha miezi miwili ijayo kujadili namna ya kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha vilivyopo baina ya nchi hizo kwa lengo la kurahisisha ufanyaji biashara.
Rais Samia ameongeza kuwa pia wamekubaliana kufungua Ofisi ya Bandari nchini Uganda ili kurahisisha na kukuza biashara kati ya Tanzania na Uganda.
Akizungumzia kuhusu Ugonjwa wa UVIKO 19, Mhe. Rais Samia amesema wamekubaliana kuanzisha kiwanda cha pamoja cha kuzalisha dawa na chanjo kwa ajili ya binadamu na wanyama kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo UVIKO-19.
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akiteta jambo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Samia ametumia fursa hiyo kumpongeza Mhe. Rais Museveni kwa kufadhili ujenzi wa Shule ya Msingi huko Wilayani Chato, Mkoani Geita na kusema kitendo hicho ni cha kuigwa kwani Mhe. Rais Museveni anatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa Tanzania.
Rais Samia amesema pia katika mazungumzo yao wamewaagiza Mawaziri wa Mambo ya Nje kufanya mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda mwezi Disemba ili kuweka mikakati ya kutekeleza makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa kwa nyakati tofauti na nchini hizi mbili.
Kwa upande wake, Rais Museveni amemshukuru mwenyeji wake kwa mwaliko na kusisitiza kwamba ushirikiano huo wa kindugu kati ya Tanzania na Uganda utaimarishwa na kuenziwa kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Mawaziri, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi waandamizi serikalini wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki, Rais Museveni amesema kuwa matayarisho ya msingi kuhusu kuanza kwa ujenzi wa mradi wa bomba hilo yamekamilika.
Mhe. Rais Museveni yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine, atashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Uganda, atatembelea Bandari ya Dar es Salaam na mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na kukabidhi shule ya msingi iliyojengwa Wilayani Chato kwa ufadhili wake.