NA GODFREY NNKO
Dkt.Called Nyamajeje Weggoro
ambaye amewahi kuwa mshauri wa uchumi wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne,
Dkt.Jakaya Kikwete, Awamu ya Tano,Hayati Dkt.John Magufuli na baadaye
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
anayeshughulikia Kanda ya Afrika Mashariki hadi alipostaafu amefariki. Kifo cha Dkt.Weggoro kimeelezwa na ndugu Gerson Msigwa ambaye ni Msemaji Mkuu wa Serikali leo Novemba 11, 2021 kuwa, ni miongoni mwa taarifa ambazo zimemuumiza moyo wake.
Inaniwia vigumu kuamini kuwa Dkt.Called Nyamajeje Weggoro hatunaye duniani. Nimepoteza Baba, Rafiki, Mshauri Kiongozi na mtu niliyemuona kuwa ni hazina muhimu ya Taifa.Kwa ufupi sana nilikutana nae Ikulu mwaka 2015 akiwa Mshauri wa Uchumi wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, baadaye akaendelea kuwa Mshauri wa Uchumi wa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kisha akateuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia Kanda ya Afrika Mashariki hadi alipostaafu.Mtu huyu alikuwa mahiri katika uchumi, mwenye uzoefu wa kiwango cha juu, aliyejiamini na kusimama kwenye hoja za kitaalamu, aliyeujua mwelekeo wa uchumi wa Tanzania na aliyesheheni ujuzi katika ushauri. Kwake yeye HAPANA ilikuwa HAPANA na NDIO ilikuwa NDIO.Nimekutana nae mwezi uliopita (Oktoba 2021) katika fukwe za Aga Khan Dar es Salaam akiwa mazoezini na mimi nikiwa mazoezini akaniambia “Bwana mdogo Msigwa, bado nimo hii napiga kilomita ya 9, mwambie jamaa yako Brigedia Jenerali Mkeremy hamniwezi nyie vijana.Ucheshi wake utabaki kwenye kumbukumbu zangu milele. Ushauri wake nitautumia wakati wote, nitaendelea kuwa mkakamavu kama alivyokuwa yeye.Kwa heri Dkt. Weggoro, tutaonana baadaye Baba. Lala salama. NITAKUOMBEA DAIMA.Pole kwa familia na wote walioguswa na msiba huu.Raha ya milele umpe eee Bwana, na mwanga wa milele umuangazie, Dkt. Weggoro apumzike kwa amani, Amina.
Taarifa zaidi zitakujia hapa Diramakini Blog, endelea kufuatilia hapa.