NA YUSUPH MUSSA
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa, Tarafa ya Kwekivu, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga wamesema hawakufikiria kama siku moja watakuja kuona barabara ya lami ikifika kijijini kwao ama wilaya hiyo ikiwa na lami.Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Mhandisi Martin Mwashambwa (kulia) akiangalia ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. (Picha na Yusuph Mussa).
Wakizungumza na DIRAMAKINI BLOG kwa nyakati tofauti, wananchi hao
wamesema wameshangaa kuona Serikali ikiweka lami kwenye baadhi ya
barabara, huku baadhi ya barabara zikitengenezwa kwa kiwango cha
changarawe kwa ajili ya kuwezesha wananchi kuweza kusafirisha mazao
yao kwa urahisi.
Mohamed Chambo (83) mkazi wa Kijiji cha Bokwa
amesema, katika umri wake hajawahi kuona lami ikiwekwa kwenye wilaya
hiyo, lakini sasa ameshuhudia ikiwekwa kwenye kijiji chake, na kusifu
Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwezesha kuwatengenezea barabara za
vijijini ili ziweze kuwasaidia kwenye shughuli zao za kila siku.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Mhandisi Martin Mwashambwa akizungumza na DIRAMAKINI BLOG kwenye eneo la ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe wilayani Kilindi ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. (Picha na Yusuph Mussa).
"Mimi nina miaka 83, lakini sijawahi kuona lami kwenye wilaya hii ya
Kilindi. Lakini sasa naona barabara ya lami inapita kwenye kijiji chetu.
Nimshukuru Rais (Samia Suluhu Hassan) na Serikali yake kwa kutuletea
lami,"amesema Chambo.
Naye Habiba Yassin ambaye ni mkazi wa
Kijiji cha Bokwa, pamoja na kujengewa barabara ya lami, pia mradi huo wa
barabara wa kilomita tano umewapa ajira hasa wanawake, kwani walijitosa
kwenye ujenzi huo kwa kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuchimba mitaro,
kuokota mizizi, kuokota mawe makubwa ambayo hayatakiwi kuwepo kwenye
ujenzi, ambayo pia wananchi waliyachukua na kuponda na kupata kokoto.
"Mradi
huu wa barabara, pamoja na kwamba umeletwa ili tuwe na barabara nzuri,
lakini sisi wakazi wa Kijiji cha Bokwa tumepata neema nyingi ikiwemo
kufanya kazi mbalimbali. Sisi kama wanawake tuliweza kuchimba mtaro
uliopo pembeni ya barabara. Pia tumeweza kuokota mawe, kusaidia mafundi
na kuweza kulipwa. Na kuna akina mamalishe wanapika chakula kwa ajili ya
wafanyakazi.
"Mimi mwenyewe nina watoto watatu, na wote wanasoma
Shule ya Msingi Bokwa. Pesa ninayopata kwenye ujenzi huu wa barabara
umeniwezesha kuwahudumia watoto wangu kwa kupata mahitaji muhimu. Hivyo
tunaishukuru Serikali kutupatia barabara hii sababu imekuja na neema
nyingi,"amesema Yassin.
Ujenzi wa mifereji ukiendelea kwenye barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe wilayani Kilindi ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. (Picha na Yusuph Mussa).
Meneja wa Wakala wa Barabara wa Mjini na Vijijini (TARURA)
Wilaya ya Kilindi, Mhandisi Martin Mwashambwa amesema, mradi wa barabara
kwa kiwango cha lami wa Bokwa wilayani Kilindi hadi Kata ya Lengatei,
Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara ni wa kilomita tano, na unatekelezwa
kwa awamu.
Mhandisi Mwashambwa amesema Awamu ya Kwanza mradi huo
unajengwa kwa mita 400, ambapo utekelezaji wake unafanywa chini ya
mkandarasi JP Traders Ltd kutoka mkoani Dar es Salaam, na utagharimu sh.
milioni 315, ambapo mradi umeanza Septemba 3, 2021 hadi Machi 3, 2022.
Ujenzi wa mifereji ukiendelea kwenye barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe wilayani Kilindi ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. . (Picha na Yusuph Mussa).
"Barabara
ya Bokwa- Lengatei ya kilomita tano, inajengwa kwa awamu. Kwa mwaka wa
fedha 2021/2022 imetengewa sh. milioni 315 kwa ajili ya kutengeneza
kipande cha mita 400, na kazi imeanza tangu Septemba 3, mwaka 2021, na
inatarajiwa kukamilika Machi 3, 2022. Lakini kutokana na kasi ya
mkandarasi JP Traders Ltd ya jijini Dar es Salaam, kazi hii inaweza
kukamilika Januari, 2022.
"Ni kweli, sisi TARURA hii ni mara yetu ya kwanza kuweka lami
kwenye Wilaya ya Kilindi. Na tutaendelea kuboresha barabara zetu kila
tutakapopata fedha kutoka serikalini. Mfano barabara ya Bokwa- Lengatei
kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imepata sh. milioni 315, lakini hatujui
mwaka wa fedha 2022/2023 itatengewa kiasi gani cha fedha,"amesema
Mwashambwa.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Mhandisi Martin Mwashambwa (kushoto) akiangalia ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kiwango cha lami kipande cha mita 400 katika Kijiji cha Bokwa, Kata ya Bokwa mjini Songe ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita tano kutoka Bokwa- Lengatei wilayani Kiteto mkoani Manyara. Katikati ni Msimamizi wa Mradi Mhandisi Vedastus Buliro. (Picha na Yusuph Mussa).
Mwashambwa amesema Wilaya ya Kilindi ina mtandao wa barabara wa kilomita 871.59. Kati ya hizo, kilomita 59.72 ni za kiwango cha changarawe, na kilomita 811.8 ni za udongo. Lakini kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetoa sh. bilioni moja kwa ajili ya kufungua barabara, na kufanyia maboresho zile za udongo kuwa za changarawe. Pia kuna sh. milioni 500 ambazo nazo zitafanya kazi ya kutengeneza maeneo korofi na makaravati ili barabara zipitike mwaka mzima.
Naye Msimamizi wa Kampuni ya JP Traders Paul Michah amesema wanakwenda vizuri japo kokoto nyembamba kwa ajili ya uwekaji wa lami na shughuli nyingine wanazichukulia mbali, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, na watamaliza barabara hiyo ndani ya muda waliopangiwa.