Ukahaba wachefua viongozi wa dini, watoa wito kwa Serikali

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

ILI kudhibiti vitendo vya watu kujiuza miili yao, Serikali imeombwa kuangalia uwezekano wa kupeleka bungeni muswada wa sheria kali itakayowabana watu wanaofanya biashara hiyo.
Ni kwa kuweka adhabu ya kifungo cha kuanzia miaka 30 na kuendelea ili kukomesha vitendo vya aina hiyo katika jamii ya Kitanzania.

Abdulaazizi Swalehe kutoka Msikiti wa Mtaa wa Unyankindi uliopo Manispaa ya Singida ametoa ushauri huo kwenye kikao cha pamoja kati ya viongozi wa dini,maafisa watendaji wa mitaa,maafisa watendaji wa kata na Jeshi la Polisi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa jeshi hilo.

Swalehe amefafanua kuwa, Serikali imeweka sheria kali za ukeketaji hivyo ni wakati muafaka sasa umefika kwa serikali kuangalia uwezekano kwa kupitia muhimili wa Bunge la Jumuhuri ya Muungano wa Tanzania kuweka sheria kali za kuwadhibiti makahaba na wale wanaojiuza miili yao kwani itasaidia kwa kiwango kikubwa kukomesha matendo hayo.

"Kama vile Serikali ilivyoweka sheria kali kwa ukeketaji ningeshauri pia zingewekwa sheria kali za kuwabana makahaba na wale wanaojiuza nadhani ingesaidia sana,kwa sababu binadamu huwa hasikii ila watu wachache wanaweza wakasikia, yule ambaye ni mwerevu,na mtu mwingine huwa hasikii mpaka aone action (matendo),aone mtu anatandikwa ndiyo atasikia,’’amesema.

Pia aliweka wazi kuwa, masheikh pamoja na mapadri hawawezi kwenda kufanya kazi ya kuwazuia makahaba au dawa za kulevya,watadharaulika na hivyo kutumia fursa hiyo kuishauri serikali kuchukua nafasi nzuri zaidi ya kukabiliana na vitendo hivyo kutokana na wao kuwa na viboko.

"Ningeshauri ninyi mngechukua nafasi nzuri zaidi maana ninyi mna viboko,mna majela,mna maaskari sasa mtu asiyesikia unaniambia nikamkamate,ni shughuli nzito,kwa hiyo ninyi mngechukua action (vitendo) kama mlivyochukua kwa wakeketaji mkasema afungwe miaka 36, nafikiri mtakomesha.’’amebainisha.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa dini kahaba anapokamatwa na kufikishwa mahakamani hutozwa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 3,000 adhabu ambayo alionyesha kutoridhishwa nayo kwa madai kwamba vitendo hivyo havitakoma zaidi ya kuendelea siku hadi siku.

‘’Leo kahaba anapokamatwa na kufikishwa mahakamani anatozwa adhabu ya faini ya shilingi elfu tatu huo ni mchezo wa kuigiza au hawa watu wa kikosi cha usalama barabarani, mtu anapomsababishia mtu mwingine kifo analipa elfu ishirini,kesho atakanyaga mtu mwingine,’’amesema na kuonyesha kushangazwa na sheria zilizopo.

Kiongozi huyo wa dini hata hivyo alipendekeza kwa serikali kuwa wakati umefika sasa wa kuzifanyia marekebisho sheria za aina hiyo kwani zimepitwa na wakati, kwani anaamini kabisa kwamba sheria za Tanzania hazina kipingamizi kufanyiwa marekebisho.

Mwenyekiti wa Dini mbalimbali Mkoa wa Singida,Hamisi Kisuke alisema baada ya kikao hicho kati ya jeshi la polisi, watendaji na viongozi wa dini kamati ya dini mbalimbali itakwenda kukaa kikao cha pamoja ili kulikemea suala la ukahaba.

‘’Sasa mimi kama mwenyekiti wa dini mbalimbali watanikubali hawa kuwakusanya tukafanye kikao cha pamoja tuweze kulikemea jambo hili kwa nguvu nyingi sana kupitia vyombo vya habari,kupitia wewe uturuhusu tukae tuweze kusema katika kikao chetu cha dini mbalimbali mkutano wetu wa kukemea ukahaba ndani ya mji wetu wa Singida,’’alisema Kisuke ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Misuna.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,ACP Stella Mutabihirwa alisisitiza kwa kuwataka viongozi hao kutoacha kuhudhuria kwenye vikao vya mapendekezo, kwani vikao vya mapendekezo ya kisheria vinaanzia ngazi ya chini.

ACP Mutabihirwa alifafanua kwamba endapo watashiriki katika vikao vya kisheria vya mapendekezo,upo uwezekano wa sheria ya wanawake kujiuza pamoja na sheria ya usalama barabarani kufanyiwa marekebisho huku akipingana na kiongozi wa dini aliyesema ukeketaji unaruhusiwa kwa madai kwamba wanaoyafahamu madhara ya vitendo hivyo vya ukeketaji ni wanawake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news