NA DOREEN ALOYCE
KATIKA kutekeleza Ilani Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025, Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) Wilaya ya Dodoma Mjini umesema wataendelea kufuatilia kwa karibu miradi ya Serikali huku wakitumia fursa hiyo kuwasaidia vijana kuweza kunufaika.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana UVCCM kupitia Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Dodoma Mjini, Said Kasote ameyasema hayo wakati alipokuwa kwenye ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Dodoma Mjini ambayo inasimamiwa na halmashauri hiyo.
Katika ziara hiyo iliwalenga Umoja wa Vijana UVCCM Mkoa wa Dodoma kutembelea Ofsi za Umoja huo ngazi ya Wilaya kwa ajili ya kuwatembeza kwenye miradi ya Dodoma Mjini kama inatekelezwa ipasavyo kupitia Ilani ya Chama Cha mapinduzi ambayo inawataka viongozi wa chama kusimamia kwa ukaribu miradi ya Serikali na jinsi gani inawanufaisha wananchi.
Kasote akizungumza kwa nyakati tofauti amesema kuwa, uongozi na timu waliyoambatana nayo wameridhishwa na hali inavyoendelea kwani wameona ni jinsi gani vijana wameshirikishwa kwenye miradi hiyo na mikopo ambayo inaenda kuwanufaisha wao na familia zao.
"Leo tumetembelea miradi ya Serikali tumeona vikundi vya vijana Kata ya Nzyuguni wakitengeneza majiko kupitia mikopo inayotolewa na Halmashauri, katika soko kuu la Job Ngugai wamepewa kipaumbele na wengine kuanzisha maduka ya simu,hoteli ya nyota tano jambo ambalo ndilo lengo la Serikali kupitia Awamu ya Sita. Sisi umoja wetu kazi yetu ni kuhakikisha tunamuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia miradi hiyo,"amesema Kasote.
Nae Katibu wa jumuiya hiyo, Ahmed Kibamba amesema miradi hiyo yenye thamani kubwa ya fedha ni kwa maslahi ya umma, hivyo alitumia fursa hiyo kuwasihi vijana kuacha dhana potofu kwamba wenye elimu ndiyo wanapewa kipaumbele kitendo ambacho kinaweza kuwasababishia kukosa fursa kutokana na mawazo yao potofu.