>BEI KUBWA VIFURUSHI VYA DATA MWIBA MAENDELEO YA KIDIGITALI TANZANIA
>Wadau walia kila kona vifurushi kupanda maradufu tena kimya kimya
>Tasnia ya habari Mitandaoni, elimu, Dini, Burudani waathirika pakubwa
KUTOKANA na kupanda maradufu kwa bei za vifurushi vya interneti nchini, huku GB 1 ya Data ikipatikana kwa zaidi ya dola 1.3 kumesababisha kupungua kwa kasi idadi ya watumiaji wa internet nchini hivyo kuathiri taasisi, mashirika na watumiaji binafsi wa interneti ambao hutumia huduma hiyo katika majukumu mbalimbali pamoja na burudani.
Aidha, kutokana na bei hizo kutokuwa rafiki kwa watumiaji wa huduma hiyo hasa mwananchi wa kawaida Taasisi na tasnia mbalimbali zimetajwa kuathirika kwa namna moja au nyingine.
Tasnia ya habari za kidigitali
Watoa huduma za maudhui katika Tovuti na programu tumishi na mtandao wa YouTube na blogs wamelalamika kutokana na kushuka kwa kasi kwa watumiaji wa huduma zao huku wakiiomba wizara na wadau husika kujadili na kulipatia mwarobaini suala hili.
Ili kuendesha mitandao ya kijamii inatakiwa kutumia bando kila wakati ili kuendelea kuuhabarisha umma kuhusu habari na matukio mbalimbali hivyo gharama kubwa za vifurushi zimekuwa kikwazo kwa bloggers & youtubers.
Tasnia ya Burudani
Wasanii na watoaji maudhui ya burudani hasa kwa mtandao wa video wa YouTube nao wamedai idadi ya wanaofuatilia kazi zao kushuka kwa kasi kwa siku za karibuni, jambo ambalo wamedai kuathiri sana kipato chao. Vilevile mitandao mbalimbali ya takwimu inaonesha kushuka kwa watumiaji wa mtandao wa YouTube Tanzania kwa siku za karibuni.
Watumiaji Binafsi
Watumiaji mbalimbali wa internet Tanzania nao wameonesha kukerwa na kupanda Mara kwa Mara kwa bei za vifurushi tena vinapandishwa kimya kimya licha ya mamlaka kusema gharama zimeshuka huku wakidai uishaji wa haraka kuliko kawaida wa vifurushi hivyo, vile vile wanakumbusha ahadi za wadau na wizara kuahidi mara kadhaa kulishughulikia tatizo hilo na kubakia ahadi hewa.
Pamoja na hayo, Bei hizi ambazo zimetajwa kutokuwa rafiki kwa watumiaji huenda zikazidi kuathiri mfumo mzima wa maendeleo ya kidigitali hasa kwa mashirika, taasisi, na makampuni kama vile huduma za kibenki za kidigitali, huduma za afya, elimu, na dini zinazopatikana kwa njia za kidigitali pamoja na tasnia ya michezo ya bahati nasibu ya mtandaoni.
Haki ya kupata taarifa, imeathiriwa
Kila mtu ana haki ya kupata taarifa, kwa miaka ya karibuni kutokana na ukuaji wa maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano hata Serikali imekuwa ikitoa taarifa zake kwa idara mbalimbali kwenda kwa wananchi kwa njia ya mitandao, hii inahusisha hata Matangazo ya moja kwa moja ya Uapisho wa viongozi, uzinduzi wa miradi na hotuba za viongozi kwa wananchi ambao wapo maeneo tofauti tofauti. Kutokana na kupanda kwa gharama za bando baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanakosa haki ya kupata taarifa hizo kutokana na bando kupaa.
Hapo awali ilikuwa rahisi mtu kuweza kufatilia mubashara matangazo mubashara ya matukio ya kitaifa kupitia mtandaoni lakini hivi sasa wananchi wengi tunapata shida kuweza kuangalia hadi mwisho matangazo hayo kwani maranyingi kabla tukio halijaisha kifurushi cha data kinakuwa kimeshaisha, hivyo athari hizi si tu kwetu wananchi ila hata kwa watoa taarifa wakiwemo viongozi wa Serikali.
Na hivyo ujumbe uliokusudiwa kuwasilishwa kwetu wananchi unakuwa umekwamishwa na gharama za vifurushi vya data.
Wadau Watoa ushauri
Wadau mbalimbali wanaishauri wizara husika, pamoja na makampuni ya simu nchini yanayotoa huduma hiyo muhimu kwa maendeleo kuangalia upya na kwa umakini jambo hili kwa maendeleo na tija ya nchi.
Tunafahamu kuwa Vifurushi vya Data ni Ofa za makampuni ya simu katika kufanya ushindani wa kibiashara lakini licha ya kuwa ni ofa basi tunashauri ziwe zenye kuleta unafuu kwa mwananchi kwakuwa pia kukiwa na huduma hizo nzuri, hata matumizi ya Mawasiliano kwa njia ya simu yataongezeka na kutaongeza mapato kwa Serikali kwa njia ya kodi na tozo zilizopo hivi sasa.
Imeandaliwa na baadhi ya watoa maudhui, waandishi wa habari za mtandaoni na watumiaji wa mitandao Tanzania
Tags
Habari