Wadhamiria kupeleka mapendekezo bungeni kuomba nyongeza ya fedha za lishe ya mtoto

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WABUNGE Vinara wa Usalama wa Chakula wamesema kwamba watapelekea mapendelezo Bungeni ili kuiomba Serikali iweze kuongeza kiwango cha fedha ya lishe ya mtoto inayotengwa kila Halmashauri ya Sh.1000 kiweze kubadilishwa badala yake wapewe kwa asilimia.
Hayo yamesemwa leo na Katibu wa Kikundi cha Wabunge Vinara wa Usalama wa Chakula, Mhe Salome Makamba ambaye alimwakilisha Mwenyekiti wa Kikundi hicho Mhe Neema Lugangira katika Mkutano wa Siku mbili wa Wadau wa Lishe.

Mkutano huo wenye kaulimbiu “Lishe Bora ni Msingi wa Maendeleo ya Mtaji wa Binadamu katika Uchumi wa Kishindani” uliowakutanisha wadau wa chakula na lishe uliofanyika jijini Tanga.

Mhe. Salome Makamba, alisema sambamba na hilo wanaomba Serikali sikivu chini ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan iweze kuangalia upya suala la kupelekea masuala ya chakula kusimamiwa na TBS badala yake isimamiwe na chombo maalumu tofauti kwa sababu TBS haiwezi kuthibitisha ubora na wakati huo huo kusimamia usalama

Katibu huyo aliiomba pia Serikali na wadau wote wakiwemo Watanzania waweze kusimamia suala la usafi na usalama wa chakula kwa sababu Tanzania ni nchi Tajiri na ina rasilimali nyingi.

“Tusimamie usalama wa chakula kutoka Shambani mpaka kwa mlaji na tuache kutupa chakula chini lakini Halmashauri zijenge vizimba ili chakula kiwepo mahali pa usalama na serikali iweze kusimamia kwenye masoko itasaidia kuweza kuwa na chakula salama na safi na kutengeneza Taifa bora,"amesema.

Aidha, amesema kwamba wanaipongeza Serikali kwa juhudi za kutengenza Sera, Kanuni na Sheria mbalimbali pamoja na changamoto zote na zipo changamoto ndogo ambazo wanaomba wafikishe ili waweze kusonga mbele kama Taifa kwa kuweka chakula salama kwenye nchi yetu na lishe bora.

Amesema, wanaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu iweze kukamilisha Sera ya Taifa ya Chakula na Lishe ambayo ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na kwa tarkibani miaka mitatu sasa ipo tu hapo Ofisini na inatakiwa kufanya Maboresho ya Sera hiyo maana imeshapitwa na wakati.

Amesema ikibidi kabla ya hawajamaliza kipindi cha Bunge wapeleke Bungeni mapendekezo ili iweze kutungiwa Sheria kama Sheria ya Usalama wa Chakula huku akiipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuandaa Mpango wa Lishe kwenye Kilimo.

Hata hivyo aliiomba Ofisi ya Waziri Mkuu wasaidie Wizara nyengine za Kisekta ziweze kutengeneza Mpango wa Lishe wa kisekta kama ambavyo Wizara ya Kilimo imefanya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news