NAIROBI-Wafungwa watatu wanaohusishwa na ugaidi ambao walitoroka jela ya Kamiti nchini Kenya siku ya Jumatatu wamekamatwa.
Watatu hao Musharaf Abdalla maarufu Alex Shikanda , Joseph Ouma na Mohammed Ali Abikar walikamatwa katika eneo la Kitui.
Kwa mujibu wa BBC, walitoroka kutoka jela inayolindwa zaidi baada kutoboa ukuta wa jela hiyo.
Baadaye walitumia nguo aina ya blanketi na waya kutengeneza kamba ambazo walitumia kupanda kuta mbili ndefu za jela hiyo.
Hatua hiyo ilisababisha baadhi ya maafisa wa jela ya Kamiti kukamatwa kwa madai ya kuwasaidia wahalifu hao kutoroka
Siku ya Jumatano, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alimwaagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, Fred Matiangi kuhakikisha wanatumia kila mbinu kuwakamata wahalufi hao hatari.
Alivitaka vitengo vyote vya upelelezi kuwawajibisha maafisa wote waliodaiwa kuhusika na kutoroka kwao.
Wahalifu hao wamekamatwa baada ya kuonekana na wakazi wa eneo hilo ambao waliwashuku watatu hao walipotaka kuoneshwa njia ya kuelekea msitu wa Boni huko kaunti ya Lamu.
Pia walionekana kuchoka na wenye kiu, walinunua maziwa mengi na maji , mkate na biskuti kutoka kwa maduka ya eneo hilo na kulipa pesa.