Walimu watoa neno kwa Halmashauri ya Meru kuhusu fedha za UVIKO-19

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WALIMU wa Shule za Sekondari zinazoteleleza miradi ya vyumba vya Madarasa 70 ya fedha za UVIKO-19 wameushukuru Uongozi wa Halmashauri ya Meru mkoani Arusha kwa kurahisisha upatikanaji wa saruji ambayo itasaidia miradi hiyo kutekelezwa kwa kasi zaidi.
"Tunamshukuru Mkurugenzi wetu na Mwenyekiti kwa kuhakikisha saruji inapatikana ukizingatia miradi hii ni mingi na inatekelezwa kwa wakati mmoja,"amesema Mwalimu Athuman Seleman ambaye ni Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Muungano.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Mwalimu Zainabu Makwinya ameendelea kuishukuru Serikali kwa kutoa Shilingi Bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo 70, ambapo halmashauri inahakikisha vifaa ambavyo havipatikani kirahisi katika maeneo miradi inapotekelezwa vinaagizwa toka kiwandani.

Ikumbukwe kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan hivi karibuni imetoa Shilingi Bilioni 1.78 kwa mchanganuo wa,Bilioni 1.4 fedha za mpango wa maendeleo dhidi ya UVIKO-19, kujenga vyumba 70 vya Madarasa katika Shule za Sekondari.

Shilingi Milioni 80 ambazo ni fedha za UVIKO -19 kwa ajili ya kujenga bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Patandi Maalum, Milioni 250 fedha za tozo za Simu kujenga Kituo cha Afya Mareu, na Shilingi Milioni 50 (fedha za tozo) kukamilisha maboma mawili katika Shule za Sekondari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news