WANAFUNZI DARASA LA SABA WASIFUTIWE MATOKEO YA MITIHANI

NA ROBERT KALOKOLA

WADAU wa elimu mkoani Geita wameliomba Baraza la Mitihani nchini (NECTA) kuangalia upya adhabu inayotolewa kwa wanafunzi wa darasa la Saba au kidato cha nne ya kuwafutia matokeo ya mitihani na kutowapa fursa nyingine ya kurudia mitihani mingine baada ya kugundua walijihusisha na udanganyifu wa mitihani yao ya taifa.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kadama katika hafla ya kupongeza walimu na wafanyakazi baada ya shule hiyo kushika nafasi ya tisa kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka huu.(Picha na Robert Kalokola).
Ushauri huo umetelewa na Dkt. Daniel Izengo, Mkurugenzi wa Shule ya Msingi Kadama, Letisia Pastory pamoja wanafunzi katika hafla ya kupongeza walimu na wafanyakazi wa shule ya msingi ya Kadama English Medium wilayani Chato Mkoa wa Geita ambayo ilishika nafasi ya tisa kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka huu.

Wadau wametoa ushauri huo siku chache baada ya NECTA kupitia kwa Katibu wa baraza hilo, Dkt.Charles Msonde wakati anatangaza matokeo ya darasa la saba ya mwaka 2021 kutangaza kufuta matokeo yote ya wanafunzi 993 nchi nzima waliobainika kujiingiza katika wizi wa mitihani.
Mdau wa ulimu Mkoa wa Geita Dkt. Daniel Izengo akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kupongeza walimu na wafanyakazi wa Shule ya Msingi Kadama. (Picha na Robert Kalokola).

Dkt.Izengo ambaye ni mmiliki wa Kituo cha Afya cha Lisbon kilicho katika Mji mdogo wa Katoro amesema kuwa, adhabu hizo zinapaswa kuangaliwa upya kwani zinaharibu mfumo mzima wa wanafunzi wanaofutiwa matokeo.

Ameeleza kuwa, wanafunzi hao mara nyingi kwa umri wao hawawezi kupanga kuiba au kuvujisha mitihani yao wenyewe bila msaada wa walimu wao au wamiliki wa shule.

Hivyo adhabu zingelenga zaidi kuwaadhibu walimu na wamiliki wa shule ili wasiingize wanafunzi wao katika njama za kuiba mitihani na badala yake wafundishe kwa bidii zaidi.

Dkt.Izengo ameomba serikali kupitia NECTA kuangalia njia nzuri ya kubana zaidi walimu ili mitihani hiyo isivujishwe na kuwahusisha wanafunzi kwa sababu kutoa adhabu kwa mtu mwisho ambaye ni mwanafunzi siyo sawa.

Amesema wanafunzi hao kulingana na umri wao wanakuwa hawajakomaa kufikia hatua ya kuiba mitihani  hivyo serikali iangalie namna mpya ya kutoa adhabu ambayo itamfanya mwanafunzi asipoteze ndoto za maisha yake.

Amesema kuwa, Shule ya Msingi Kadama imekuwa mfano wa kuigwa kwa kuandaa wanafunzi kwa jitihada za walimu na kufaulu mitihani bila kujiingiza katika vitendo vya wizi wa mitihani ya kitaifa.

Amesema kuwa, amekuwa akifuatilia wanafunzi wanasoma katika shule hiyo na kujiridhisha kuwa wanakuwa na maarifa ya kutosha hivyo matokeo ya mwaka huu ameona atoe zawadi kwa watumishi wote wa shule hiyo.

Dkt.Izengo ametoa zawadi ya milioni moja kwa shule hiyo ili iongeze tanki la maji ili wanafunzi waendelee kupata muda wa kujisomea ili wasihangaike na kutafuta maji kwa mbali.

Aidha, ametoa zawadi ya fedha taslimu ya elfu hamsini (50,000) kwa kila mfanyakazi wa shule ambao jumla yao ni 41 kuwapongeza kwa ushirikiano wa kufanya kazi kwa bidii na kuchangia shule hiyo kupata nafasi ya tisa (9) kati ya shule 11,909 kitaifa.
Mkurugenzi wa shule ya msingi Kadama Letisia Pastory. (Picha na Robert Kalokola).

Naye mmiliki wa shule ya Kadama English Medium Letisia Pastory amesema, adhabu hizo zina madhara makubwa kwa mwanafunzi anyefutiwa matokeo na badala yake serikali iimarishe zaidi udhibiti ili mitihani isivujishwe.

Amefafanua kuwa, hata pale inapotokea NECTA wakatoa fursa ya pili ya wanafunzi hao kurudia mitihani kwa msamaha baada ya kufutiwa,wanafunzi hao hawafanyi vizuri kwa sababu wanakuwa wamesha kata tamaa na kupata msongo wa mawazo wa kufutiwa matokeo.

Aidha, amesema kuwa hata shule ikipewa adhabu ya kutolewa mitihani, adhabu hiyo inaathiri hadi wanafunzi moja kwa moja kwa sababu wanafunzi wanaosoma kwenye shule hiyo hawatahiniwa.

Shule ya msingi Kadama ambayo ipo kata ya Buseresere Wilaya ya Chato imeshika nafasi ya tisa kitaifa na nafasi ya pili Kimkoa na nafasi ya kwanza kiwilaya katika matokeo ya darasa la saba mwaka huu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Makigo Makigo amesema kuwa shule hiyo ina historia ya kupata matokeo mazuri katika mitihani ya darasa la saba.

Ametaja matokeo ambayo yalikuwa mazuri zaidi kuwa ni mwaka 2018 ambapo shule hiyo ilishika nafasi ya 1 kitaifa na kupata mwanafunzi wa kwanza kitaifa na mwanafunzi wa kumi kitaifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news