NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Wananchi wa mkoa wa Mwanza wameaswa kubadili mtindo wa maisha ikiwemo kuacha kula vyakula vya Sukari kwa wingi, kufanya mazoezi, kuacha kuvuta tumbaku ili kujiepusha na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel wakati wa kufunga maadhimisho ya siku ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza iliyofanyika viwanja vya CCM Kirumba wilaya ya Ilemela kwa mkoa wa Mwanza na kupambwa na kauli mbiu ya _BADILI MTINDO WA MAISHA KUEPUKA MAGONJWA YASIYO AMBUKIZA_
"Utafiti uliofanyika mwaka 2012 unaonesha katika watu 100 wenye umri wa miaka 25 na zaidi 9% wana Kisukari, 34% wana uzito uliopindukia, 23% Wana wingi wa mafuta kwenye damu sababu ya mtindo wa maisha,"amesema.
Aidha,Mkuu huyo wa mkoa amempongeza Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla Kwa maandalizi mazuri ya shughuli hiyo huku akihimiza wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Mhe Hasan Elias Masalla amemhakikishia Mkuu huyo wa mkoa kuwa wilaya yake Kwa kushirikiana na wadau wataendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kufanya mazoezi ya kukimbia na viungo yanayoendeshwa Kila wiki la pili la Kila mwisho wa mwezi
Nae mganga Mkuu wa wilaya ya Ilemela Chacha Marwa amewaasa wananchi kuchukua hatua dhidi ya ugonjwa wa Kansa ya Mlango wa Kizazi kwa kujitokeza katika vituo vya kutolea huduma kujua afya zao na kujipatia matibabu
Maadhimisho ya siku ya magonjwa yasiyoambukiza yametanguliwa na shughuli ya Mbio za Km 8 kutokea uwanja wa CCM Kirumba kupitia Kitangiri, Daraja la Furahisha, Mwaloni Kirumba, Kirumba polisi na kuhitimishwa Tena katika uwanja wa CCM Kirumba na upimaji wa hiari wa magonjwa mbalimbali ya kuambukiza.