NA ANGELA MSIMBIRA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe.Ummy Mwalimu ameziagiza Sekretarieti za Mikoa zote nchini kuhakikisha wanasimamia, wanazishauri na kutoa maelekezo kwa halmashauri katika kutekeleza miradi ya maendeleo
Akiongea na Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa, Waziri Ummy amesema Sekretarieti za Mkoa zina wajibu wa kuzisimamia halmashauri na kuhakikisha halmashauri zinatekeleza majukumu yao ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Waziri Ummy amesema, Sekretarieti za Mikoa nchini ndio kiungo muhimu katika kuhakikisha miradi ya halmashauri inatekelezwa kwa wakati na inalengo ya kutatua kero za wananchi
Amewaelekeza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa na kupokea maelekezo na kuyatekeleza kwa wakati ili kuleta maendeleo katika Mikoa yote nchini
"Ninawategemea sana Sekretarieti za Mikoa katika kuhakikisha wa akagua miradi ya maendeleo nayotekelezwa na halmashauri kwa kuwa nyinyi ndio kiungo. Muhimu katika utekelezaji wa miradi,"amesema Waziri Ummy.
Amewataka kuhakikisha wanasimamia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri kwa kukagua na kusimamia utekelezaji miradi hiyo.
Amezitaka Sekretarieti za Mikoa kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za serikalli ili ziweze kutumika katika kutatua kero za wananchi.