NA MARY MARGWE
IWAPO wataalam wa afya na maafisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri wakifanikiwa kutoa elimu ya haki ya afya ya uzazi salama kikamilifu kwa wanawake na wasichana itawasaidia sana kuwabadilisha kisaikolojia na kupata ujasiri katika kuripori taarifa za vitendo vya ukatili wanavyokutana navyo.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Manyara (MNRPC ), Jaliwason Johnson alipokuwa akizungumza na DIRAMAKINI BLOG juu ya mradi wa kuwapatia elimu hiyo wanawake na wasichana.
Johnson ambaye ndiye mratibu wa mradi huo amesema hayo baada ya kuona kuwa walengwa wakubwa wanaokutana na ukatili huo ni wanawake, wasichana ambao kila kukisha wamekua wakikutana na matukio mbalimbali ya vitendo vya ukatili.
Aidha, amesema kufuatia kuwepo kwa vitendo hivyo kwa kundi hilo Klabu ya Waandishi wa Habari Manyara ( MNRPC ) iliandika andiko kwa Shirika la Women Fund Trust (WFT) kuomba ufadhili wa kushirikia nao kuwezeshwa kuwafikia walengwa hao kwa kutoa elimu juu ya haki ya afya ya uzazi salama kwa kundi hilo.
" Kwanza kabisa nipende kuwashukuru Women Fund Trust (WFT ) kwa kutukubalia andiko letu na kutuwezesha kupata shilingi milioni 10 kwa ajili ya kutekeleza mradi huu kwa kipindi cha miezi sita ambapo baada ya kupata fedha za kutuwezesha kufanyika kwa huo mradi tukawashirikisha wataalam wa afya na Maafisa Ustawi wa Jami kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' na Babati ili kuweza kutoa elimu hiyo kwa wanawake na wasichana,"amesema Mratibu wa mradi huo.
Aidha, amesema wapo akina mama waliokuwa wakifanyiwa ukatili mkubwa, lakini walishindwa na kuopoga kutoa taarifa wakiogopa kutengwa na familia na wengine wakiona aibu kuripoti matukio wakidhani wanajidhalilisha, na wengine kwenda mbali zaidi wakiona kusema matendo hayo kama ya kubakwa ama kulawitiwa ni kutengeneza laana katika familia.
Amesema, wapo wanawake waliokuwa wakipitia changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutelekezwa na waume zao huku wakiendelea kulea mimba hadi mtoto mwenyewe, lakini pia wapo wanaobeba mimba ambazo walikuwa hawajaridhiana na waume zao, hivyo kupitia mradi huo utakwenda kuwezesha kujengewa uwezo wa kuweza kukabiliana na matukio hayo ya ukatili dhidi yao.
Afisa Ustawi wa Jami wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Mathias Focus akitoa elimu kwa walengwa wa mradi wa haki ya afya ya uzazi salama Kata ya Riroda wilayani humo hivi karibuni. (Picha na Mary Margwe).
Akiongea na DIRAMAKINI BLOG, Rehema Bulambo (45 ) amesema, kesi nyingi kama za kubaka na kulawitiwa huwa hazifiki mwisho kwa kisingizio cha upelelezi bado unaendelea, hapo ndio sehemu inayowakatisha watu wengi tamaa ya kuendelea kuripori matukio haya na kuamua kukaa kimyaa.
"Hapa Afisa Ustawi wa Jamii ametuelimisha kuwa tusikae na matukio ya ukatili tuendelea kuripori matukio mbalimbali ya ukatili likiwepo na ubakaji na kulawitiwa unasema twende polisi kweli watu wanakwenda polisi, lakini kila ukifika polisi unaambiwa upelelezi bado unaendelea, utafuatilia upelelezi utapiga kwata polisi hata miaka miwili bado unaambiwa upelelezi bado unaendelea, baadaye unaona shughuli zako zote zinakwama shambani hakuendeki, nyumbani hakukaliki ndipo unaamua kuchoka na kukata tamaa ya kuendelea na kesi unaicha, ndipo baadaye polisi wanageuza kibao wanasema mmemalizana kinyumbani kumbe mtu amechoka kurudirudi kule polisi huku ushahidi wote ulishakamilika, chakushangaza unaambiwa upelelezi unaendelea, hapa kuna tatizo kubwa sana tusaidiwe,"amesema Bulambo.
Naye Afisa Afya wa Hospitali ya Tumaini ya Wilayani Hanang mkoani Manyara, Anasia Mariki amesema asilimia 12 ya wanawake wanaopata watoto ni kati ya umri wa miaka 15 -19, hivyo wanatakiwa waelimishwe kujua lazima wafahamu kilicho mbele yao kulingana na umri walionao katika umri wa unaostahili kuzaa.
"Hata ukiangalia katika maeneo yetu tunayotoka, wasichana wadogo wadogo wa miaka 17, 18 na 19 unakuta tayari wameshaolewa na wana watoto, na ndio maana tunawaelimisha hata namna ya kutumia uzazi wa mpango utakaowezesha kupishanisha umri wa watoto wakati wa kujifungua,"amesema Afisa afya huyo.
Afisa Ustawi wa Jami Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, Martha Sulle alisema wapo wanawake wanaokwenda kuripoti matukio ya ukatili wamepigwa na wengine hata kupatwa majeraha makubwa na makovu ya maisha, huku wengine hata kupata na ulemavu, chakushangaza bado wengine wanashindwa kutoa taarifa hizo.
Hata hivyo Sulle alibainishwa baadhi ya maeneo makuu ambayo watoto hubakwa na kulawitiwa kuwa wakati wanafunzi wanaporudi nyumbani, wanapokuwa machungani kuchunga mifugo na wengine pale wanapotumwa kufuata mahitaji dukani njiani ndipo hukutana na matukio hayo ya kikatili.