Watendaji watakiwa kusimamia ubora ujenzi wa madarasa

NA FRED KIBANO 

SERIKALI imewaasa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara kusimamia ubora na thamani ya fedha na kuhakikisha kwamba majengo ya vyumba vya madarasa yanakamilika kwa wakati.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange ametoa kauli hiyo wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Sengenya iliyopo wilayani Nanyumbu.

Dkt.Dugange amesema, katika mwaka ujao 2022 hakutakuwa na machaguo ya pili na tatu na ndiyo maana Serikali imeamua kuwekeza kwenye miundombinu ya vyumba vya madarasa kote nchini ili kuhakikisha kila mototo wa kitanzania anasoma masomo ya elimu ya sekondari kwa kuanza pamoja mara shule zinapofunguliwa.

Amesema, Serikali imewekeza fedha kwenye miradi bila kuwasumbua wananchi kuchangia kama zamani ambapo mchakato wake ulikuwa unachukua muda mrefu sana. Amewaasa Watendaji wa Halmashauri ya Nanyumbu kuongeza kasi ya ujenzi baada ya kujionea kasi yao kuwa ndogo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mheshimiwa Mariam Chaurembo amesema katika robo ya pili ya mwaka 2021/22 Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu ilipokea kiasi cha shingi Bilioni moja na milioni 240 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya madarasa kwenye shule 16 za sekondari na shule 2 shikizi.

Aidha, amesema changamoto kubwa waliyokumbana nayo ni pamoja na uhaba wa maji na idadi ndogo ya mafundi wa kufyatua matofali yenye viwango.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu, Bw. Emanuel Kapinga amesema, shule hiyo ilipokea milioni 160 kwa ajili ya kujenga vyumba vinne vya madarasa na mpaka sasa fedha imekwishatumika na salio ni shilingi milioni 97 kwa kazi zilizobakia na kwamba ujenzi unaendelea vizuri japo upo katika hatua tofauti.

“Ujenzi wa madarasa mawili yapo katika hatua ya ufungaji wa lenta, madarasa matatu yapo katika hatua ya kuta na madarasa matatu mengine yapo kwenye hatua ya kuanza kujenga ukuta,"amesema.

Serikali ilipeleka fedha za ustawi wa jamii na kukabiliana na Uviko-19 kwenye halmashauri zote nchini ili kupunguza au kuondoa kabisa uhaba wa miundombinu ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wote wanaanza kidato cha kwanza pamoja na hivyo kuondoa dhana ya kuwepo machaguo ya pili na tatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news