NA MWANDISHI DIRAMAKINI
Serikali imeombwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na madhehebu ya dini kudumisha pamoja na kutunza malikale zilizopo kwenye maeneo mbalimbali ili kumbukumbu za siku za baadaye ziweze kupatikana na kushuhudiwa na vizazi vijavyo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wazee wenye Umri wa Miaka Sitini na kuendelea (WAYUSUFU) Usharika wa Askofu Emmanueli, Richard Ghamunga Nkuwi ameyesema hayo kwenye ziara ya kutembelea majengo ya zamani likiwemo jengo lililojengwa mwaka 1917 lililopo Kijiji cha Ruruma wilayani Iramba ambalo kwa sasa limekuwa gofu ili waweze kulikarabati upya.
Nkuwi amesema kwamba endapo serikali italitambua jengo hilo lililojengwa mwaka 1917 itakuwa ni jambo jema iwapo itachangia nguvu zake kwa lengo hilo la kuunga mkono umoja huo ambao umeona kuna umuhimu wa kulifufua ili vizazi vijavyo viweze kujua historia ya kijiji hicho.
Amesisitiza kwamba Kijiji cha Ruruma kilichopo mji mdogo wa Kiomboi ndiyo kitovu cha elimu,afya hivyo halina budi kutambuliwa pamoja na kuenziwa kwa hali na mali na uongozi wa serikali ya Mkoa wa Singida.
"Na Wakristo wote wenye mapenzi mema na wanadamu wote wenye mapenzi mema watusaidie,lakini na serikali yetu ikijua jambo hili kwamba lipo itusaidie ituunge mkono ili kudumisha,kutunza hizi mali kale ambazo zipo Ruruma na zingine ambazo zinaweza zikaonekana katika Dayosisi yetu ya Kati,"amesisitiza Mwenyekiti huyo wa WAYUSUFU.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Historia ya WAYUSUFU, Damiano Mkumbo ameshauri kuwa malikale zilizopo katika Kijiji cha Ruruma zitambuliwe kwa kuwekwa alama ili kuepusha jamii inayozunguka kijiji hicho kutovamia kwenye maeneo hayo ya malikale.
‘’Lakini tuna mali kale zingine ambazo zinaweza kutumika kuipaisha zaidi Singida,sasa mimi kwa maoni yangu naona hizi malikale tulizoziona leo zitambuliwe kwa kuwekwa alama ili kuepusha jamii inayozunguka kijiji hiki kutovamia kwenye maeneo haya ya malikale,’’amefafanua Mkumbo.
Msaidizi wa Askofu Kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKT) Dayosisi ya Kati,Sypriani Hilinti pamoja na kuupongea mpango wa umoja huo wa WAYUSUFU wa kuokoa gofu la Ruruma,lakini hakusita kusisitiza pia kwamba kijiji hicho ndicho chanzo cha elimu,afya,kitovu cha kiserikali kikanisa (kidini),hivyo linapaswa kuenziwa na Mkoa wa Singida.
Hilinti ameshauri pia kuwa ombi lililotolewa na mmoja wa waumini wa Kijiji cha Ruruma kwamba umoja wa WAYUSUFU hauna budi kuanzishwa katika dayosisi yote ili kuongeza nguvu za kusaidiana kwa shughuli mbalimbali za kiroho.