NA TITO MSELEM-WM
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko ametoa wito kwa wamilki wa Migodi ya kuchimba na kuchakata Madini ya Ujenzi ya Kokoto kufuata Taratibu na Sheria zilizowekwa na Serikali.
Waziri Biteko amesema hayo, alipotembelea migodi ya Kerai Construction, Even Enterprises, Gulf concrete pamoja na Saint Maria inayojishughulisha na uchimbajii wa Madini ya ujenzi ya Kokoto iliyopo katika eneo la Lugoba wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Waziri Biteko amesema, migodi yote inayojishughulisha na uchimbaji wa kokoto katika eneo la Lugaba lazima ziandae mpango wa ufungaji wa mgodi baada ya kumaliza uchimbaji (Mining Closure) na uwasilishwe Tume ya Madini kwa ajili ya kusimamia utekelezaji.
Aidha, Waziri Biteko amezitaka Kampuni zote zinazochimba na kuchakata Madini ya Ujenzi ya Kokoto kuhakikisha zinaandaa mpango wa kuchangia huduma za maendeleo kwa jamii inayowazunguka (CSR) kulingana na vipaumbele vya eneo husika.
“Kuchangia huhuma za maendeleo kwenye maeneo yanayozunguka migodi si jambo la hiari bali ni takwa la kisheria, hivyo niwaombe mkae na Mkurugenzi pamoja na Mkuu wa Wilaya ili mjue vipaumbele vya wilaya katika kuchangia huduma za maendeleo kwa jamii inayowazunguka,” amesema Waziri Biteko.
Katika hatua nyingine, Waziri Biteko amempongeza Mwekezaji wa Kampuni ya Kerai Construction Limited, Dipin Patel kwa kuongeza ajira kwa vijana wa eneo la Lugoba na Msata, kuchangia huduma za maendeleo kwa jamii inayowazunguka mradi pamoja na kulipa maduhuli ya serikali kwa kutumia mfumo wa mashine za kielektroniki (POS).
Pia, Waziri Biteko ametoa wito kwa kampuni zote zinazojishughulisha na uchimbaji wa Madini ya Ujenzi kuhakikisha zinalipa maduhuli ya Serikali kwa kutumia mfumo wa POS ili kupata taarifa sahihi za mauzo na kudhibiti udanganyifu kwenye makusanyo ya mapato ya Serikali ambapo wachimbaji wasio waaminifu walikua wakifanya udanganyifu kwenye hati za mauzo ya vitabu.
Sambamba na hilo, Waziri Biteko amesema wapo baadhi ya watu ambao wamevamia kuchimba madini ya dhahabu katika mto Wami ambapo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Abdala pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani Ally Maganga kuhakikisha wachimbaji hao wanaondolewa katika eneo hilo ambalo ni chanzo cha maji.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dar es salaam na Pwani Ally Maganga amesema eneo la Lugoba na Msata lina jumla ya Migodi 32 ambapo wa sasa migodi 19 tu ndiyo inayofanya kazi, migodi 13 imesimamisha uzalishaji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo changamoto ya soko hali inayo changiwa na kukosekana kwa miradi ya ujenzi hususan katika jiji la Dar es Salaam.
Maganga amesema, takwimu zinaonesha kuwa uzalishaji wa kokoto kwenye eneo la Lugoba na Msata ni wastani wa tani 2,400,000 hadi tani 2,640,000 kwa mwaka ambapo Serikali hukusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.0 hadi bilioni 3.5 kwa mwaka.