NA TITO MSELEM-WM
WAZIRI wa Madini Doto Biteko amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga Zabibu Napachu kuhakikisha Soko la Madini la Wilaya ya Kilindi linafunguliwa katika eneo la mgodi wa Seita ili wachimbaji wasisafiri umbali mrefu kwenda kuuza madini yao.
Waziri
Biteko amesema hayo, alipotembelea mgodi wa Seita uliopo Kata ya
Kikunde kijiji cha Chamtui wilayani Kilindi mkoa wa Tanga ambapo
amekagua shughuli za uchimbaji madini na kuzungumza na wachimbaji wadogo
wa madini ya dhahabu katika mgodi huo.
“Afisa
Madini, ndani ya wiki moja kuanzia leo uhakikishe Soko la Madini la
Wilaya ya Kilindi linafunguliwa katika eneo hili la wachimbaji na baada
ya kufungua soko, asiruhusiwe mtu yoyote kusafirisha madini bila
kupita Soko la Madini la Kilindi ili kudhibiti otoroshaji na kuisaidia
Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kupata mapato yake,” amesema Waziri
Biteko.
Pia,
Waziri Biteko amewataka wanunuzi wote wa madini (brokers) katika mgodi
wa Seita kuhakikisha wananunua madini kwa bei elekezi ambayo inapangwa
na Tume ya Madini kutokana na Soko la Dunia la siku husika.
Aidha,
Waziri Biteko amesema kuna Sheria ya Ardhi na Sheria ya Madini, hizi ni
Sheria mbili tofauti, kuna baadhi ya watu wanazichanganya hizi Sheria
na wengine wanazani madini yakiwa kwenye ardhi yao basi madini hayo ni
mali yao, hapana madini ni mali ya Serikali haruhusiwi mtu yoyote
kuyachimba mpaka awe na leseni.
“Kiongozi
na Msimamizi Mkuu wa Sekta ya Madini nchini ni Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan na sisi Wizara ya Madini
ni wasaidizi wake,” amesema Waziri Biteko.
Waziri
Biteko amesema Rais Samia Suluhu Hassan anataka awaone wachimbaji
wadogo wanatajirika kupitia shughuli zao za uchimbaji na wanashiriki
kikamilifu katika uchumi wa madini ambapo anataka aone utulivu kwenye ya
uchimbaji wa madini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi Aberi Busalama amesema wilaya yake haijanufaika ipasanyo na uwepo wa madini wilayani humo kwa sababu ya kukosekana kwa soko la kuuzia madini katika wilaya hiyo ambapo madini yanayopatikana hupelekwa kuuzwa wilaya jirani ya Handeni, hivyo kukosa mapato yatokanayo na madini na kuchochea utoroshwaji wa Madini.
Pamoja na mambo mengine, Busalama amemuomba Waziri Biteko kupeleka Afisa Migodi Mkazi katika wilaya ya Kilindi ili awasaidie wachimbaji wadogo mbinu bora za uchimbaji na kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira na uchimbaji salama pamoja na kudhibiti utoroshaji wa madini wilayani humo.