Waziri Mkenda aanza ziara ya kikazi nchini Uganda

NA MATHIAS CANAL

WAZIRI wa Kilimo,Prof. Adolf Mkenda amewasili Mjini Entebbe nchini Uganda kwa ziara ya kikazi ya siku nne kuanzia Novemba 23, 2021 hadi Novemba 26, 2021 ambapo atapata fursa ya kujifunza mafanikio ya kilimo bora cha michikichi.

Ziara hiyo ni mualiko wa kampuni ya Wilmar International kwa ajili ya kwenda kujifunza kilimo cha Michikichi nchini Uganda kwa utaratibu wa (Block Farming) unaowaunganisha wakulima na viwanda vya kukamua mafuta ya kula ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano na kampuni hiyo na Wizara ya Kilimo, mara baada ya kukutana kwenye vikao kazi nchini Tanzania vilivyojadili namna kampuni hiyo inavyoweza kuwekeza kwenye tasnia za mazao ya mafuta ya kula ikiwemo michikichi, alizeti na maharage ya soya.Katika ziara hiyo Waziri Mkenda ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye, Mkurugenzi wa Maendeleo Mazao wa Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu na wataalam wengine wa kilimo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Waziri Mkenda atakutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Uganda, Mhe. Frank Kagyigyi Tumwebaze, kadhalika atafanya ziara kwenye kiwanda cha kampuni ya Wilmar International ambayo imeonyesha nia kuwekeza kiwanda cha mafuta ya kula kwa ubora wa mwisho kutokana na uzalishaji wa michikichi, alizeti na maharage ya soya nchini Tanzania. Waziri Mkenda amesema kuwa, ili uwekezaji huo uwe na tija uhakika wa malighafi ni suala muhimu ikiwa ni pamoja na kuwa na mfumo bora wa uzalisaji kama vile mashamba makubwa (Block Farming) yanayowahusisha wakulima wadogo.

Amebainisha kuwa, kwa upande wa Michikichi kampuni hiyo ingependa kuanzisha mashamba ya pamoja yenye ukubwa wa angalau ekari 10,000 kwa kila shamba. Kampuni hiyo ya Wilmar inamiliki mashamba katika nchi mbalimbali ikiwemo Uganda, Indonesia na Malaysia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news