>Atoa kipindi cha mpito cha kusafirisha Vinia hadi Juni 30,2022
NA LUSUNGU HELELA-WMU
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameruhusu kusafirisha makontena 187 ya Vinia kwenda nchi za nje yaliyokuwa yamekwama bandarini baada ya kutoa tamko la kuzuia usafirshaji malighafi za mazao ya misitu kwenda nchi za nje ikiwemo Vinia.
Plywood ndiyo inayotumika katika shughuli za ujenzi wa maghorofa na kutenganisha vyumba katika ofisi, licha ya kuruhusu usafirishaji wa makontena hayo 187 yaliyokuwa na Vinia, Dkt. Ndumbaro ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutoruhusu uvunaji na biashara ya gundi ndani na nje ya nchi mpaka pale watafiti watakapotoa hasara na faida yake.
Waziri Dkt. Ndumbaro ametoa ruhusa hiyo leo Novemba 24, 2021 wakati alipokuwa akizungumza na wafanyabishara wa mazao ya misitu katika mkutano ulioitishwa na wafanyabiashara hao jijini Dar es Salaam kupitia Baraza la Taifa la Wafanyabishara (TNBC) wakiomba kuongezewa muda wa kusafirisha mazao hayo.
Akifafanua ruhusa hiyo, Dkt.Ndumbaro amesema, ruhusa hiyo inahusu makontena 187 tu ambayo yapo tayari yameshafika bandarini na sio kwa makontena ambayo hayako bandarini.
''Naomba nieleweke vizuri ruhusa hii ya kusafirisha vinia itahusu makotena 187 tu ambayo nyaraka zake tayari zilishawasilishwa kwenye vyombo vya kiserikali,'' amesisitiza Dkt.Ndumbaro.
Katika hatua nyingine, Serikali imewaongezea muda wafanyabiashara wa mazao ya misitu nchini kusafirisha Vinia kuanzia leo hadi tarehe 30 Juni 2022 kwa vigezo na masharti kuzingatiwa.
Akitaja masharti hayo, Dkt.Ndumbaro amesema, wafanyabiashara watakaoruhusiwa kusafirisha vinia kwa kwa kipindi hicho tajwa watatakiwa kuwasilisha mpango kazi wa kuleta mashine ya kuchakata Vinia hadi hatua za mwisho pamoja na kuwasilisha taarifa za kodi na malipo mengine ya Serikali.
Mbali na mashariti hayo, Dkt. Ndumbaro amesema, wafanyabiashara hao ili waweze kuruhusiwa kusafirisha mazao hayo watatakiwa kuwasilisha taarifa za haki za wafanyakazi katika viwanda vyao pamoja na gharama halisi za mzigo huo.Hata hivyo, Dkt. Ndumbaro ametoa onyo kwa mfanyabishara yeyote atakayetoa taarifa za uongo na akathibitika hatapewa ruhusa ya kusafirisha Vinia hiyo huku akisisitiza kuwa katika kipindi hicho cha mpito yeye mwenyewe Waziri ndiye aatakayehusika na kutoka vibali kwa wafanyabishara vya kuruhusu kusafirisha vinia kwenda nchi za nje.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Taifa la Wafanyabaishara (TNBC), Ben Sulus amemshukuru Waziri kwa kukubali ombi la wafanyabishara hao la kuongezewa muda huku akisisitiza kuwa ni muda muafaka sasa kwa Wafanyabishara hao kuungana kwa pamoja kuleta mashine ambazo zitachakata vinia hozo hadi hatua za mwisho ili kutoa ajira kwa wananchi wanaozunguka misitu hiyo.
Naye Mfanyabishara wa Kiwanda cha Vinia cha Yu lin, Ben Makombe amesema,wizara ina lengo jema, lakini wanaomba kuongezwa muda takribani miaka mitatu ili waweze kukusanya fedha kwa ajili ya kununua mashine ambazo zitaweza kuchakata Vinia hizo hadi hatua za mwisho.
Amefafanu kuwa mashine hizo zinauzwa dola 8,000 hivyo zinahitaji wafanyabaishara wenye mitaji mikubwa hivyo endapo watapewa muda wataweza kuzinunua.