NA MWANDISHI MAALUM,WAMJW
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi amesema, Wizara hiyo imeamua kuachana na Mkandasi Wakala wa majengo (TBA), aliyekuwa anajenga Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, kutokana na kusuasua kwa ujenzi huo kwa zaidi ya mwaka sasa ambapo ujenzi umesalia katika ngazi ya msingi pamoja na Serikali kulipa zaidi ya bilioni 1.04.
Prof. Makubi amesema, hata hivyo Mkandarasi huyo anapaswa kurejesha kiasi cha shilingi milioni 968 kama ilivyoainishwa katika hati ya malipo ya mwisho sambamba na kuagiza kukamilishwa haraka mchakato wa zabuni ya mkandarasi mpya na kuwasilisha nyaraka za mkataba wa mpya wa ujenzi ili kuombea fedha Wizarani kwa ajili ya kuendeleza mradi huo ambao ni muhimu kwa huduma za uzazi na mtoto.
Akiwa anaendelea na ziara yake katika Hospitali hiyo Prof. Makubi ameonekana kusikitishwa na kitendo cha kutofungwa kwa wakati mashine ya kuzalisha hewa ya Oksijeni (Filling station), na kuagiza mkandarasi mbobezi aliyepewa kazi hiyo kuhakikisha ameanza kufunga mashine hiyo ifikapo Novemba 21, mwaka huu.
Ziara hiyo ya Prof. Makubi ilimfikisha katika jengo la radiolojia ambalo litafungwa mashine ya CT-Scan na kupigwa butwaa na mlango wa chumba hicho ukiwa ni mwembamba kiasi mashine hiyo haiwezi kupita huku akiagiza watumishi wa Wizara ya afya waliosimamia ujenzi huo kuhakikisha wanapata fedha za kupanua mlango huo hata kama ni kwa kukatwa katika mishahara yao.
Akiwa anahitimisha ziara yake katika Hospitali hiyo ya Mkoa, Prof. Makubi ametoa ushauri kwa viongozi wa mkoa wa Geita kujenga jengo moja litakalotoa huduma jumuishi za Jengo la Idara ya dharura (EMD) na Wagonjwa wa uangalizi maalum (ICU) katika Hospitali ya rufaa ya mkoa huo ili kuokoa fedha na kuepusha wananchi kutembelea umbali mrefu kufuata huduma hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinategemeana.
Katibu Mkuu, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto yupo katika ziara kwenye Mikoa ya Kanda ya Ziwa kukagua shughuli mbali mbali za Afya katika kanda hiyo.