NA MWANDISHI DIRAMAKINI
WIKIENDI imefikia tamati kwa wenyeji Dodoma Jiji FC kulazimishwa sare ya bila kufungana na Coastal Union.
Ni katika mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao umepigwa usiku wa Jumapili ya Novemba 28, 2021 katika dimba la Jamhuri jijini Dodoma
Matokeo hayo yanawafanya Dodoma Jiji kufikisha alama 12 na kurejea nafasi ya tatu, wakati Coastal Union inatimiza alama nane na kusogea nafasi ya saba baada ya wote kucheza mechi saba.
Novemba 27, 2021 wao Tanzania Prisons ambao walikuwa wenyeji walipata ushindi wa pili mfululizo katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Ni baada ya kuichapa Namungo FC mabao 3-1 katika dimba la Nelson Mandela lililopo mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.
Mabao yote ya Tanzania Prisons yamefungwa na mshambuliaji Jeremiah Juma dakika ya nne, 11 na 26, wakati bao pekee la Namungo FC limefungwa na mshambuliaji Mrundi, Bigirimana Blaise dakika ya 68.
Kwa upande wa wenyeji Mbeya City walilazimishwa sare ya 2-2 na KMC FC Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Mabao ya Mbeya City yalifungwa na Paul Nonga dakika ya nane na Richardson Ng'ondya dakika ya 67 na ya KMC yalifungwa na Matheo Anthonyu dakika ya 13 na Mohamed Samatta dakika ya 86.
Awali, Ruvu Shooting wameibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa uwanja wao wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Mabao ya Ruvu yalifungwa na Zuberi Dabi dakika ya 30 na Rashid Juma dakika ya 84, wakati la Kagera Sugar limefungwa na Ally Nassor dakika ya 84.