NA GODFREY NNKO
UONGOZI wa Klabu ya Yanga umekubaliana na maamuzi ya Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) kutupilia mbali kesi yao dhidi ya winga Mghana, Bernard Morrison.
“Matokeo ya kesi hii hayatoirudisha nyuma klabu ya Yanga katika kupambania haki zake pale itakapoona inafaa kufanya hivyo,”imesema taarifa ya Mwenyekiti wa Yanga, Dkt. Mshindo Msolla.
Awali taarifa ya CAS ilisema kwamba mkataba wa awali wa Yanga na Morrison ulimalizika Julai 14, mwaka 2020 na wa pili ambao Mghana huyo anaukana alisharejesha fedha za klabu hiyo dola za Kimarekani 30,000 hivyo hakuna kesi baina yao.
Aidha, uamuzi huo unafikiwa baada ya mashabiki wa Yanga SC na Simba SC kwa muda mrefu kurushiana vijembe kutokana na kila mmoja kuvutia upande wake wakiamini kuwa, upande mmoja una haki zaidi ya mwingine.
Kwa nyakati tofauti, mashabiki wa Simba SC wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, ushindi huo si wa Morrison pekee bali kwa klabu nzima, hivyo kutoa pongezi kwa uongozi na mchezaji huyo kwa hatua waliyofikia.