NA GODFREY NNKO
UBAO wa mitanange ya Ligi Kuu Tanzania Bara (Ligi Kuu ya NBC) leo Novemba 30,2021 umeonesha matokeo ya furaha kwa baadhi ya mashabiki huku upande wa pili wakisononeka.
Ni baada ya Wanajwangwani, Yanga SC ambao walifika Nyanda za Juu Kusini na kufanikiwa kulitumia vema dimba la Sokoine lililopo jijini Mbeya ambapo wamefanikiwa kupeleka kilio kwa Mbeya Kwanza kwa kuichapa mabao 2-0.
Matokeo hayo yanaweza kuwa na faraja kwa Kocha Nesrdin Nabi ambaye awali alionekana kuwa na wasiwasi kuhusu hali ya dimba hilo.
Wakati huo huo,Biashara United wamelazimishwa sare ya 1-1 na Polisi Tanzania. Ni katika mtanange ambao umepigwa katika dimba la nyumbani la Karume mjini Musoma mkoani Mara.
Adam Adam aliwatanguliza wageni, Polisi dakika ya 46, kabla ya Nassib Mpapi dakika ya 61 kurejesha hali ya amani kwa kutundika mchomo mmoja nyavuni.
Matokeo ambayo yanaifanya Biashara United kufikisha alama nane na kusogea nafasi ya saba, wakati Polisi Tanzania inafikisha alama 11, ingawa inabaki nafasi ya tano baada ya timu zote kucheza mechi saba.
Pia shambuliaji Mkongo, Idris Mbombo dakika ya 52 ameipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mwendelezo wa mitanange hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ushindi huo ambao umepatikana katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam umeifanya nyota ya wenyeji kung'ara leo
Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kufikisha alama 10 na kusogea nafasi ya sita, wakati Mtibwa Sugar inabaki na alama zake mbili baada ya timu zote kucheza mechi saba na kuendelea kushika mkia katika Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga SC walifanyaje?
Saido Ntibanzokiza dakika ya 17 alitundika bao safi kwa adhabu ndogo ya mpira wa kutenga baada ya kiungo Feisal Salum kufanyiwa madhambi nje kidogo ya eneo la 18 na Fiston Mayele akawainua mamia ya mashabiki wa yanga SC katika dimba la uwanja wa Sokoine dakika ya 25 baada ya kuunganisha pasi safi ya Feisal Salum.
Awali Wanajangwani walianza mchezo kwa kasi ya chini, lakini hadi dakika za kipindi cha kwanza zinafikia tamati ubao ulikuwa unasoma mabao 2-0 dhidi ya Mbeya Kwanza FC.
Katika kipindi cha pili Mbeya Kwanza walionekana kutulia na kucheza kwa kushambulia ila safu ya ulinzi ua YangaSC ilikuwa imara na kumaliza mchezo huo bila ya kuruhusu bao.
Mchezo huo unakuwa ni wa kwanza kwa Mbeya Kwanza kupoteza kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine na mchezo wa pili kwao kupoteza katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.