HARARE, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema linahiataji dola milioni 65 ili kupunguza ukosefu wa usalama wa chakula nchini Zimbabwe.
WFP ambalo ni Shirika la Umoja wa Mataifa limesema tathimini yake imeonyesha kwamba zaidi ya watu milioni 5 katika taifa hilo wanatarajia kushuhudia uhaba wa chakula katika miezi ijayo.
Msemaji wa WFP nchini Zimbabwe, Belinda Popovska ameiambia VOA kwamba, shirika hilo limeanza kuangalia namna ya kupata ufadhili kwa ajili ya kuagiza chakula kwa wale wanaohitaji.
Belinda anasema, ripoti za karibuni za mwaka huu katika maeneo ya vijijini nchini Zimbabwe, iliyotolewa na kamati ya tathmini imeashiria kwamba kiasi cha watu milioni 2.9 ambao ni sawa na asilimia 27 ya kaya wataendelea kukumbwa na ukosefu wa chakula wakati wa kipindi cha baada ya mavuno, Januari na Machi mwaka 2022.
Katika maeneo ya mijini,hadi watu milioni 2.4 walitarajiwa kutokuwa na chakula cha kutosha kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa karibuni kwenye maeneo ya mijini mwaka huu wa 2021.
Serikali inasema Zimbabwe mwaka huu imepata mavuno mengi, lakini ukosefu wa chakula katika maeneo ya vijijini unaashiria kuwa mavuno kwa hakika hayakuwa makubwa hivyo.
Waziri wa Habari nchini Zimbabwe, Monica Mutsvangwa amesema, uhaba wa chakula nchini humo utamalizika kukiwa na uzalishaji zaidi mashambani katika msimu ujao wa mwaka 2021/2022 ambao unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Ameongeza kuwa serikali itahakikisha kuwa wakulima wana bidhaa za kutosha na fedha wanazohitaji ili kukidhi mahitaji ya wote, binadamu na matumizi ya viwandani.
Zimbabwe iliwahi kuwa mzalisihaji mkubwa wa chakula katika eneo hilo,lakini kwa miaka mingi imekabiliwa na uhaba wa chakula, na kulazimishwa kutegemea misaada ya taasisi za kibinadamu kama World Vision, USAID na WFP ili kuwalisha watu wake.
Picha na The Guardian.
Tags
Kimataifa