NA DENNIS GONDWE, DAR
BENKI ya CRDB imeshauriwa kujenga makao makuu yake jijini Dodoma ilikiwa ni kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma na kustawisha makao makuu.
Ushauri huo ulitolewa na Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aisha Masanja alipokuwa akiongea na maofisa waandamizi wa Benki ya CRDB katika ukumbi wa mikutano wa benki hiyo jijini Dar es Salaam, baada ya timu ya kimkakati ya uwekezaji na masoko ilipotembelea makao makuu ya CRBD.
Afisa Mipango Miji Jiji la Dodoma, Aisha Masanja (wa kwanza kulia) alielezea fursa za uwekezaji Jiji la Dodoma katika kikao na maafisa waandamizi wa Benki ya CRDB katika ukumbi wa mikutano wa benki hiyo.
Masanja alisema kuwa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepanga Mji wa Dodoma na kupima viwanja kwa ajili ya uwekezaji.
Amesema, ni wakati muafaka kwa Benki ya CRDB kufikiria kwenda kuwekeza Dodoma kwa kujenga makao makuu.
“Zaidi ya kuwekeza kwa kujenga makao makuu yenu, pia mnaweza kwenda kupanga katika majengo ya Halmashauri ya Jiji yaliyokamilika katika Mji wa Serikali na kusogeza huduma za kibenki katika mji huo,”alisema Masanja.
Akiongelea fursa za viwanja kwa watumishi wa Benki ya CRDB na wananchi kwa ujumla, Masanja alisema kuwa, zipo fursa nyingi za kununua viwanja vya makazi.
“Tunavyo viwanja vya makazi katika maeneo mbalimbali ya halmashauri, mfano eneo la Ipala, Mtumba, Ihumwa na Kikombo. Wafanyakazi wanaweza kuona ni gharama kulipa kwa mara moja lakini kwa kupitia taasisi tunaweza kukubaliana njia bora ya kulipa viwanja ili wafanyakazi waweze kunufaika na kushiriki katika ustawishaji wa makao makuu,”alisema Masanja.
Kwa upande wake, Mpima Ardhi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Leonard Machunde aliitaja benki hiyo kuwa ni kubwa ikiwa na wateja ambao ni wawekezaji kwenye viwanda.
“Nitumie fursa hii kuwakaribisha sana wawekezaji ambao ni wateja wa Benki ya CRDB kwenda kuwekeza katika Jiji la Dodoma. Hata wanaotaka kuongeza ukubwa na wigo wa huduma zitolewazo katika viwanda vyao hapa Dar es Salaam tunawakaribisha,” alisema Machunde.