Dawa za kulevya si rafiki mwema, tumkatae

NI wazi kuwa, miongoni mwa vitu hatari au marafiki hatari katika maisha ya sasa ni pamoja na utumiaji au uuzaji wa dawa za kulevya.
Dawa za kulevya ni kemikali ambazo ziingiapo mwilini huathiri ubongo wa mtumiaji na kumsababishia kuwa na matendo, hisia, fikra na muonekano tofauti na matarajio ya jamii.

Kemikali hizi hutokana na mimea na madini ambayo ni mali ghafi muhimu kwa mahitaji mengine ya mwanadamu. Dawa hizi huingia mwilini kwa njia kuu tatu:

>Njia ya kunywa / kula
>Kuvuta na
>Kujidunga sindano

Miongoni mwa dawa hizo ni pamoja na bangi, mirungi, cocaine, heroin na mandrax.

Kwa nini dawa za kulevya si rafiki mwema? Kwa sababu rafiki mwema hawezi kukuingiza katika matatizo ya kiafya,kiuchumi na kimaisha kama zilivyo dawa za kulevya.

Rafiki mwema ni yupi na vipi vigezo vya rafiki mwema.

DIRAMAKINI BLOG tunaamini kuwa, sifa moja wapo ya rafiki mwema ni mshauri mwema. Kigezo hiki dawa za kulevya hazina badala yake ukizitumia utajikuta zinakupa hisia au kuushauri ubongo wako utende mambo ambayo ni hatari katika maisha yako,jamii na Taifa kwa ujumla.

Sifa nyingine ya rafiki mwema ni kushirikiana na wewe nyakati zote za shida na raha, kamwe matumizi ya dawa za kulevya hayawezi kukupa ushirikiano huu badala yake yataendelea kukutumbukiza katika tabu,shida, maangaiko na karaha.

Rafiki mwema pia anasikiliza maoni yako ,ushirikiano katika kazi, mpole na mwenye upendo wa dhati,mkarimu na yupo tayari kwa lolote juu yako iwe katika shida na raha na mengine mengi ambapo utumiaji au uuzaji wa dawa za kulevya hauna sifa wala kigezo hata kimoja.

DIRAMAKINI BLOG inaamini kuwa, vijana hawana sababu ya kuendelea kujihusisha na rafiki muuaji na asiyekuwa na huruma katika maisha, dawa za kulevya si tu ni mwanzo wa kukupotezea malengo ya maisha bali muuaji.

Kwa kukataa utumiaji wa dawa za kulevya na biashara ya dawa hizo, ndipo tutakapoliwezesha Taifa letu la Tanzania kusiwe na dawa za aina yoyote.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali kuhakikisha vijana wanakuwa salama, ndiyo maana imekamata tani 356 za dawa za kulevya kuanzia mwaka 2017 hadi 2021.

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Bw. Gerald Kusaya aliyabanisha hayo hivi karibuni alipozungumza na wanahabari kuhusu mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Mamlaka toka kuanzishwa kwake mwaka 2017 hadi kufikia mwishoni mwa Septemba 2021 kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilifanikiwa kukamata jumla ya watuhumiwa 45,784 wa dawa za kulevya, kilogramu 356,563.1 za dawa za kulevya pamoja na kuteketeza ekari 628.75 za mashamba ya bangi.

Vijana kwa umoja wetu tusimame imara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kupiga vita utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya nchini, tutambue kuwa sisi ni nguvu kazi ya Taifa.
#kataadawazakulevya_timizamalengoyako

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news