NA MWANDISHI MAALUM
ERICK Omondi ambaye ni mchekeshaji maarufu ndani na nje ya Kenya ameutumia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram kuzungumza na mashabiki wake kuhusu mapambano yake dhidi ya kurudisha hadhi ya muziki nchini humo.
Kupitia mazungumzo aliyoyaita hotuba kwa taifa, Omondi amesema kuwa, yeye ni mtu mwenye ushawishi na nguvu kubwa Afrika Mashariki.
Amesema, kutokana na nguvu hiyo ndio sababu ya kujihusisha na harakati mbalimbali za ukombozi wa sanaa ya Kenya inaoonesha viashiria vya kuyumba.
Aidha,kufuatia kampeni yake ya kutaka wasanii wa Kenya wapewe kipaumbele zaidi ya wasanii wengine kutoka nje ya taifa hilo,Omondi amewataka Wakenya kususia tamasha litakalofanyika hivi karibuni.
Ni ikiwa waandaaji hawatatii ombi lake la kubadilisha mabango yanayowaonyesha wasanii wa Kenya kama bidhaa ndogo sokoni na wageni kuonekana wenye thamani zaidi.
Tamasha la Desemba 12 la AFRO-VASHA litakalopambwa na baadhi ya wasanii kutoka nchini Tanzania akiwemo Harmonize, Omondi amesema haliwatendei haki wasanii wa Kenya, hivyo yafaa Wakenya walisusie.
Mbali na Harmonize, wasanii wengine ni Nameless, Wahu, Hart The Band, Ssaru, Bey T, Iyanii, Mixmasterlenny,DJ Dii, DJ Malaika, DJ LISNEY na DJ Slahver ambao watatumbuiza mubashara katika tamasha hilo mjini Naivasha, Kenya.