NA ASILA TWAHA
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Bi. Mwanahamisi Ally amesema fedha za UVIKO -19 na tozo za miamala ya simu zimeelekezwa katika miradi ya afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Amesema hayo mapema wiki hii alipokuwa akikagua miradi inayoendelea iliyotokana na fedha za Uviko-19 na tozo za miamala ya simu na kueleza kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa imepokea shilingil bilioni 2.9 kutekeleza miradi hiyo.
Ameendelea kufafanua bilioni 1.660 zimeelekezwa kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari ambapo vyumba vya madarasa 83 vitajengwa katika shule 22.
Amesema Shule ya Sekondari Mount Igovu ilikuwa na changamoto ya upungufu wa madarasa sababu ya uwepo wa wanafunzi wengi lakini ameeleza kwa pesa za UVIKO – 19 walizo pokea zitawasaidia kuweza kuongeza madarasa katika shule hiyo na wanafunzi hao kuweza kukaa vizuri na walimu pia kuendelea kutoa elimu vizuri zaidi.
“Shule ya Mount Igovu imejengewa madarasa 2 ambapo kila darasa limegharimu shilingi milioni 20 mpaka linakamilika na likiwa na viti na meza na fedha hizi zimetokana na fedha za Uviko-19," amesisitiza.
Akielezea fedha za tozo za miamala ya simu Bi. Mwanahamisi Ally amesema kuwa, wameshapokea shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga kituo cha Afya cha Ipera na Iwondo amesema vituo hivyo vikikamilika vitasaidia kutoa huduma kwa wakazi wa Mpwapwa na maeneo jirani.
“Tunaishukuru Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia miradi tunaahidi kuisimamia mpaka ikamilike kwa ubora na wakati niwaombe watendaji wenzangu tuendelee kutekeleza majukumu yetu wananchi wanatutegemea kwa ajili ya kutoa huduma bora,” amesema.
Kwa upande wa msaidia fundi Happy Kaungu ameishukuru Serikali kwa kutumia “Force Account” ujenzi wa shule hizo zimewapa ajira ya kujenga na kupata fedha na kuendelea kuhudumia familia.