NA MWANDISHI DIRAMAKINI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani imewapatia mikopo wanavikundi ambao ni wajasiriamali kutoka ndani ya wilaya hiyo ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka (2018) ikiwataka kutenga asilimia 10 ya fedha inayotokana na mapato ya ndani.
Akifungua mafunzo, Mhe. Shabani Manda Mwenyekiti kamati ya uchumi aliwapongeza wataalamu kwa kuweza kufanikisha zoezi la utoaji wa mikopo katika vikundi vilivyotimiza vigezo vya kupata mkopo huo huku akisisitiza fedha kutumika sawa na malengo waliyojiwekea wana kikundi wote na sio kuzigawana kwa mtu mmoja mmoja.
Akiendelea Mhe. Manda aliwataka wanufaika wa mikopo hiyo kurejesha kwa wakati ili iweze kuwasaidia wengine ambao wapo kwenye foleni ya kuomba mikopo
"Mikopo mnayopewa sio zawadi wala fadhila huu ni mkopo kama mikopo mingine inayotolewa na mabenki, mmepata neema ya kuwa sehemu ya mikopo hiyo hivyo mjitahidi kurejesha ili kujenga uaminifu utakaowafanya mkopeshwe tena pale inapobidi,"alisema.
Mohamed Mwera Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya amempongeza Mkurugenzi Mtendaji Bi. Mwantumu Mgonja kwa kuendelea kusimamia agizo la OR TAMISEMI la utenga asilimia 10 ya fedha zitokanazo na mapato ya ndani kwa ajili ya kuwezesha maendeleo ya wana Mkuranga na Wilaya nzima, Mhe. Mwera amevisistiza Vikundi ambavyo vimepata Mkopo kuwa na tabia ya kuhudhuria mafunzo ya elimu kwa wajasiliamali yanayotolewa ndani na nje ya Wilaya ili kujijengea uwezo katika shughuli zao za ujasiriamali.
Naye Afisa biashara, Bw.Mohamed Kiguga amewataka wajasiriamali wote kujua ni aina gani ya huduma wanayoifanya ili kumsaidia kujua nia na lengo ya huduma yake kwa wateja na pia kuwataka kutafuta masoko watakayoweza kuuza bidhaa zao hizo hasa kupitia wadhamini, mitandao ya kijamii, vipeperushi nk ilikuweza kuongeza masoko ya kupata ya bidhaa zao ndani na nje ya Wilaya.
Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri imetenga kiasi cha sh. 684,139,840 kwa ajili ya kukopesha vikundi vya vijana,wanawake na Watu wenye ulemavu ambapo kwa awamu ya kwanza kiasi cha sh. 400,000,00 kimetolewa kwa vikundi 36 ambapo vikundi vya wanawake 16, Vijana 11 na walemavu 9 kati ya hivyo vikundi 4 ni vya kilimo, vikundi 7 vya ufugaji na uvuvi vikundi 16 ni vyenye asili ya viwanda na vikundi 9 ni vya usafirishaji.