NA GODFREY NNKO
SERIKALI ya Israel kupitia Ubalozi wake nchini Rwanda imechangia Franka (Rwf) 100 milioni (zaidi ya shilingi za Kitanzania milioni 220) kwa ajili ya kununua kompyuta na vifaa vingine vya walimu ambao shule zao zimeunganishwa kwenye mtandao wa intaneti kupitia Mradi wa Madarasa Mahiri (Giga).
Wanafunzi wakifurahi matokeo ya Mradi wa Giga katika moja ya shule nchini Rwanda. (Picha na UNICEF).
Mpango wa GIGA unatoa fursa kwa Rwanda kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa urahisi ikiwa lengo ni kufikia ajenda ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kwa njia pana zaidi ya kimtandao.
Giga ulizinduliwa mwaka 2019 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kwa lengo la kuunganisha kila shule duniani na itaneti ifikapo 2030.
Kama mwenyekiti mwenza wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya UNBC (United Nations Broadband Commission), Rwanda iliunga mkono mpango huo na mwaka 2020 na ilichaguliwa kuongoza utekelezaji wake barani Afrika.
Akizungumzia ufadhili huo, Balozi wa Israel nchini Rwanda, Ron Adam amepongeza hatua ambayo sekta ya elimu ya Rwanda imepiga kwa miaka mingi huku akibainisha kuwa Israel ina furaha kuunga mkono lengo kuu la nchi hiyo la kuunganishwa shule zote kupitia mawasiliano ya intaneti ili kurahisha ufundishaji.
“Elimu ndio msingi wa kila kitu, na hii inaendana na ubora. Katika enzi hii, huwezi kuzungumza juu ya ubora huku ukiondoa teknolojia.Tunaamini kwamba usaidizi huu kutoka Israel utakuwa hatua nyingine kwa Rwanda kutimiza azma yake ya kuunganishwa kwa shule na kuwa na uchumi unaotegemea maarifa,"amesema Balozi Ron Adam.
Kwa mujibu wa UNICEF, katika shule 63 ambako mradi wa Giga unajaribiwa, ni asilimia 29 tu ya kompyuta zinazohitajika na vifaa vingine vinavyopatikana, hivyo zinahitajika jitihada zaidi kuvipatia vingine.
"Tunashukuru Ubalozi wa Israel nchini Rwanda kwa usaidizi huu mkubwa kwa mpango wa kuunganisha Giga nchini Rwanda. Itawezesha ununuzi wa kompyuta mpakato za walimu katika shule zinazounganishwa na mtandao kote nchini.
"Ufadhili huu pia unakuja kupunguza pengo la ufadhili na kuziba mgawanyiko wa kidijitali katika shule, jambo ambalo ni kikwazo katika mazingira bora ya kujifunza,”amesema Julianna Lindsey, Mwakilishi wa UNICEF nchini Rwanda. (NTR)