NA MWANDISHI MAALUM
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewataka wananchi kupuuza taarifa za baadhi ya watu waliowaita matapeli ambao wamekuwa wakiwalaghai wananchi fedha zao kwa kigezo cha kuwapa nafasi za kazi katika jeshi hilo.
Msemaji wa jeshi hilo, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda ameyasema hayo Novemba 30,2021wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema, vitendo hivyo vimeleta usumbufu ambapo matapeli hao husingizia viongozi, makamanda wa jeshi kwamba wametumwa wakusanye hela ili kuandikisha vijana hao.
"Niwaombe Watanzania wawapuuze na kamwe wasidanganyike kutoa fedha ili kupata nafasi Jeshini, hakuna nafasi ya kuingizwa jeshini kwa kutumia mgongo wa fedha na nitoe rai kwa wanaofanya vitendo hivyo vya ulaghai waaache," amesema Luteni Ikonda.
Akieleza namna wanavofanya kazi, Luteni Ikonda amesema matapeli hao wanakodi gesti na kukusanya vijana kisha kuwadanganya kuwa watawapa kazi jeshini na baada ya hapo wanawatelekeza
“Wazazi wanakuja jeshini kuulizia kwa mkuu wa majeshi na wakiambiwa lete hiyo namba ukipiga inajibiwa haipatikani,"ameongeza Luteni Ikonda.
Luteni Ikonda amesema,jeshi lina taratibu na miongozo yake kwa vijana wanaotaka kujiunga na sio kigezo cha fedha kama ambayo matapeli hao wamekuwa wakifanya.