KAMPENI YA TUNAJIPANGA YAENDELEA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA UPUNGUFU WA UMEME

NA MWANDISHI MAALUM

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), linaendelea kufanyia kazi Changamoto ya upungufu wa umeme inayotokana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuanza utekelezaji wa miradi ya upanuzi wa Kinyerezi I utakaozalisha megawati 185 na Ubungo III utakaozalisha megawati 112.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Maharage Chande, Desemba 15, 2021 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 51 wa Baraza kuu la Wafanyakazi unaoendelea mkoani Morogoro.

"Tunaendelea kuchukua hatua na kuongeza
jitihada za kuhakikisha inapotokea upungufu wa mvua unaoathiri uzalishaji basi athari za moja kwa moja za upungufu wa umeme zisijitokeze nchini," amesema Maharage.

Aidha, tayari mkataba umesainiwa kwa Mradi wa Kinyerezi I kwa ajili ya upanuzi na kufikia Mwezi Aprili 2022 kituo kitaanza kuingiza kwa awamu megawati 60 kwenye gridi ya Taifa.
Ameongeza kuwa, mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere utakaozalisha megawati 2115 utakapokamilika utaondoa tatizo la uhaba wa umeme nchini.

Akizungumzia suala la upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana na ukame uliochangia mitambo ya maji kushusha uwezo wa uzalishaji umeme, amesema hali imeanza kuwa nzuri kwa hivi sasa japokuwa bado tatizo halijakwisha kabisa .

“ Tumeona maeneo ya Kilombero, Morogoro mvua zimenyesha na kwa mfano bwawa la Kidatu ambalo linategemea maji kutoka Mtera na mito midogo ukiwemo Iyovi, kina cha maji kimeanza kuongezeka, “ amesema Maharage.
Amesisitiza wateja watarajie hali ya umeme kuimarika zaidi na kwamba kutakuwa na mifumo itakayomuwezesha mteja kufanya maombi ya umeme bila kufika kwenye ofisi za TANESCO.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Luth John amesema, Serikali ya wilaya na mkoa kwa pamoja zitaendelea kushirikiana na TANESCO katika kupambana na wezi na waharibifu wa miundombinu ya shirika kwani wanalisababishia shirika hasara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news