NA ADELADIUS MAKWEGA
NILIPEWA taarifa kuwa Wizara ya Eliumu na Mafunzo ya Ufundi wana nafasi za kazi za ualimu kwa wale walio na Stashahada ya Ualimu.
Kwa kuwa nilikuwa Dar es Salaam tuliwasha Volkswageni yetu (mgongo wa chura) hadi Magogoni ambapo wizara hii ilikuwepo. Nilipofika hapo niliambia kuwa kwa sasa saa moja na nusu asubuhi si muda wa kutoa huduma kwa wageni wanaotoka nje ya wizara huduma hiyo hadi saa tatu kamili.
Kweli nilitii maelekezo hayo ya mlinzi wa getini, ambaye yeye huwa ni mpokeaji tu wa maelekezo kutoka kwa wakubwa. Mlinzi huyu aliniamba kuwa kijana unaweza kukaa pale chini ya mwembe kuungoja muda ufike. Niliitika ndiyo kwa kichwa, kwa kuwa tulikuja na gari nilirudi kumueleza mdogo wangu ambaye alikuwa akiendesha gari hiyo kukuu, nikamwambie atafute sehemu ya kupaki gari hilo na aningoje maana mimi huduma hadi saa tatu kamili asubuhi kama nilivyoelezwa na mlinzi.
Nikiwa chini ya mwembe nilijiuliza swali kama wizara inayosimamia elimu kazi ya kuhudumia wageni kutoka nje inaanza saa tatu, je huko shuleni hali itakuwaje? Nilibakia nalo moyoni.
Saa tatu ilipofika nilielekezwa kwenda idara ya uajiri ambapo nilikutana na Ndugu Mwenda.
Ndugu huyu aliomba vyeti vyangu nikamkabidhi na akaniambia sawa andika barua sasa hivi, nikafanya hivyo nilipomkabidhi aliisoma na kuandika maneno katika barua hiyo akaniambia kesho njoo uchukue barua yako.
Ndugu huyu alikuwa mtu mwadilifu sana, hakuwa mtu wa tamaa na hata walimu wezangu kadhaa ambao walifika ofisini hapo siku hiyo kabla yangu na baada yangu walipata ajira hizo.(Sifahamu ndugu huyu kama amestaafu au bado ni mtumishi wa umma.)
Kwa hali ya wakati huo ajira nyingi zilikuwa zikitolewa kwa kujuana ambayo ni changamoto ya miaka mingi kwa taifa letu. Lakini Ndugu Mwenda konakona na ujanjaujanja yalikuwa ni maneno yasiyo na pahala pa kuishi katika moyo na nafsi yake, Mungu ambariki popote alipo.
Siku iliyofuata nilifika hapo saa saba mchana nikafika getini kwa mlinzi kwa kuwa aliniona jana aliniuliza
“Vipi Mwalimu umerudi tena?”. Nilimjibu kuwa ni kweli nimerudi tena, naenda kwa Ndugu Mwenda naambatana na huyu mdogo wangu. Mlinzi huyu alisema sawa hakuna neno. Sukuharibu wino wala karatasi ya serikali kuandika jina langu kitabuni, hilo lilifanyika kwa hekima ya mlinzi huyu.
Kwa bahati nzuiri Ndugu Mwenda alishakamilisha kila kitu, shule alishanipangia na akisema Mwalimu Makwega wewe unakwenda Isimani Sekondari huko Iringa Vijijini, Mkoani Iringa.
“Shule hiyo haina mwalimu ya Kiingereza na Kiswahili naomba uwende ukawasaidia Watanzania wenzetu.”
Nikamjibu sawa. Siku hiyo ndugu yangu niliyekuwa naye tangu siku iliyotangulia nayeye alitaka kuona mambo ya ofisi za serikali yalivyo, kwa hiyo niliambatana naye, kama nilivyokwambia hapo awali.
Basi nilikuwa naye pembeni, ndugu yangu huyu. Yeye ni mrefu na wakati huo alikuwa kijana sana huku akiwa na nywele nyingi kama usimpomfahamu vizuri unaweza kumuona kuwa ni msomali lakini wala.
Ndugu Mwenda alitoa maelekezo kuwa barua yako ipo masijara nenda kaichukue, kweli tulienda huko maana Ndugu Mwenda alisema kuwa huko imeenda kufunguliwa faili ambalo lina vyeti vya shule na nakala ya barua za kupangiwa kituo, moja itatumwa kwa mkuu wa shule, nyingine ya faili na moja yangu mwenyewe, ambayo nilipaswa kupewa.
Tulipofika hapo nilitumia saa zaidi ya mbili kusubiria barua hiyo huku wahusika wakiwa bize na mambo mengine. Ndugu yangu huyu alishangazwa na hali ile huku akisema kumbe ndivyo huduma zilivyo. Hapo hali haikuwa nzuri, tulitamani barua hiyo ingetolewa na Ndugu Mwenda lakini yeye alishamaliza kazi yake, shida ni kupata nakala yangu na nikaripoti Isimani.
Baada ya saa na ushehe tukimwomba mama huyu kutupatia barua uvumilivu ulitushinda huku mama huyu akidai kuwa tusimsumbue.
Maneno haya yalimkwaza ndugu yangu niliyeambatana naye akamwambia
“Mama kama ungekuwa haupo katika ofisi hii ya umma wala tusingekusumbua, ungekuwa kwako unafanya shughuli zako binafsi, unampikia mumeo wala usingetuona, lakini kwa kuwa upo hapa kwenye ofisi ya umma, mama tuvumilie na tuhudumie!.”
Kweli ilitubidi kurudi kwa Ndugu Mwenda na yeye kwenda masijara hiyo ya Wizara ya Elimu na kuingia na kuomba faili na kupewa akaichukua bahasha na kuiweka nakala yangu na mimi kuondoka zangu.
Nilipofika nyumbani nilifunga mizigo yangu na kuelekea huko Iringa. Nilipofika Isimani Tarafani nilipokelewa na kupangiwa masomo ya kusomesha.
Shule hii haikuwa na mwalimu wa somo la Kiswahili kwa hiyo tangu kidato cha kwanza hadi cha nne. Kulikuwa na wanafunzi wa kidato cha Pili walikuwa hawajasoma kabisa somo la Kiswahili mwaka mzima tangu Kidato cha Kwanza na wakati huo wlaikuwa wameingia Kidato cha Pili.
Na hata hawa wa kidato cha tatu na cha Nne nao hali haikuwa nzuri, kwa hiyo nilimshirikisha mwalimu wa taaluma nikakubaliana nae kuwafundisha baadhi ya mada pamoja yaani Kidato cha Kwanza na Pili na Kidato cha Tatu na cha Nne, nakumbuka kuwa mwalimu wa taaluma wa shule hiyo wakati huo alifahamika kama Lambet Mdeke(Mwalimu Mdeke).
Namna tulivyokuwa tunafundisha ilikuwa: Kwa wale Kidato cha Kwanza na Cha Pili mathalani mada ya Ufahamu na Utungaji zilifundishwa kwa pamoja kulinga muhtasari wa vidato hivyo viwili. Kwa Kidato cha Tatu na Nne kwa mfano mada ya uchambuzi wa Vitabu vya Mashairi-mathalani Mashairi ya Chekacheka mada hiyo walifundishwa pamoja kama muhtasari ya vidato hivyo ulivyo.
Katika hali hii ya kuwasomesha iliwanufaisha zaidi wanafunzi wa kidato cha kwanza na tatu kwa kuwa hawakuwa na mitihani ya taifa, hivyo walijianda vizuri kwa mitihani yao ya taifa mwaka uliofuata.
Kwa Kidato cha Pili na Cha Nne ilikuwa ni kuokoa jahazi tu linalozama angalau waweze kupata alama katika mitihani yao ya mwisho kwa kuwa tayari walishapitwa na muda, huku wakifundishwa hadi saa za jioni na Jumamosi.
Hicho kilichokuwa kikifanyika kilikuwa sawa na watu wanaopanda mlima pamoja nia sote kupanda na kuumaliza mlima huo pamoja. Sote tufike kileleni kwa pamoja, kwa hiyo tukiwa tunaupanda huo mlima kila mmoja wetu anahakikisha hamuachi mwenzake nyuma hili tufike kileleni pamoja. Shabaha ikiwa kufika kileleni pamoja.
Zamani iliaminika kuwa kabla Baraza la Mitihani la Taifa Kutunga mitihani ya mwisho lilikuwa likiomba kutoka kila mkoa namna kila shule ilivyofikia kufundisha kila somo hilo alafu zinatazamwa hizo mada ndipo unatafutwa wastani na mtungaji wa mtihani atatunga kulinga na wastani wa kitaifa wa mada zote zilizofundishwa, kwa somo husika kwa mwongozo wa muhtasari.
Mathalani kwa somo Basic Mathematic kwa mtihani wa kidato cha nne labda somo hilo tangu kidato cha Kwanza hadi cha Nne lina mada 35.
Ukitafutwa wastani wa shule zote za Tanzania labda wastani wa Iringa mada 30, Tanga mada 29, Kigoma mada 31, Mjini Magharibi mada 28 unatafutwa wastani wa mada hizo kwa mikoa yote labda wastani unakuwa mada 30.
Kwa hiyo mtungaji atatunga tangu mada ya 1-30 kulingana na wastani. Kwa hiyo yule aliyemaliza mada ana nafasi ya kufanya vizuri. Iwe kwa darasa la nne, la saba, kidato cha pili, cha nne na hata cha sita.
Kwa Kidato Pili na Cha Nne wanafunzi wa Isimani kulingana na kisa cha kupanda mlima tulikuwa tunawashika mkono ili tuweze kupanda nao mlima na kufika nao kileleni pamoja bila ya kumuacha hata mmoja. Kwa hiyo Baraza la Mitihani likitunga huo mtihani hata kama wastani ukiwa juu au chini kama shule imemaliza mada ya masomo yake basi mwanafunzi anaweza akaokota.
Hapa sasa dhana ya kuwapa nafasi kila mmoja ndiyo ndana ya kupanda mlima na kufika kileleni pamoja, ndiyo FALSAFA YA ELIMU KWA WOTE.
Falsafa ya elimu kwa wote ndiyo falsafa ya elimu ya Tanzania, haya ni mawazo ya Mwalimu Julius Nyerere. Kwa dhana hii kama mwalimu amefundisha akabaini kuwa wapo wanafunzi darasani hawakumuelewa inashauriwa kutumia (remedial classes) kuwaelewesha zaidi wanafunzi hao.
Mwalimu huyo kwenye Andalio la Somo anaweza akawataja kwa majina wanafunzi hao na akawafundisha wanafunzi hao saa za ziada. Ili kesho akiingia darasani kufundisha mada mpya hawa waliosoma kwenye remedial class watakuwa na uelewa sawa na wale walioelewa mapema.
Ndiyo kusema kwa sasa Watanzania wanatambua umuhimu wa masomo ya saa za ziada ndiyo maana wazazi wenyewe wanagharamia. Masomo haya yalikuwa sawa na remidial classes. Kama ni gharama Bodi/Kamati za Shule zinakubaliana na wazazi wenyewe ambayo ni jukumu lao kama miongozo ya elimu inavyosema.
Masomo ya haya hayana maana kwa mtoto wa mkubwa anayesoma shule zenye walimu wa kutosha,zenye maabara, shule za matajiri zenye.
Serikali kuu haipaswi kuingilia suala hilo bali kama kuboresha mazingira wawachie Serikali za Mitaa chini ya Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya ili waboreshe hayo mazingira kwa kusikiliza maoni na maamuzi ya Bodi/Kamati za shule zenyewe.
Kumekuwa na dhana ya wanafunzi kushiriki michezo, hilo halina shaka, Je michezo ipi? Kwideee? Kula Mbakishie baba? au Michezo ya kujifiucha ? nadhani haina umuhimu mkubwa kama elimu.
Shida iliyopo kwanza, walimu wa baadhi masomo hasa kwa sayansi na hesabu hawapo, maabara hazipo na nyingi hazijakamilika, serikali inawajibu kuhakikisha hilo linatatuliwa mapema.
Pili hata hao walimu waliopo wengi hawataki kuishi vijijini kwa kuwa hakuna utaratibu wa walimu kuhama kwa mzunguku kama zamani wakati wa ujamaa. Mtumishi alikuwa anakaa eneo moja miaka mitatu alafu anahamishiwa. Kwa sasa mtu akipangiwa kijijini ndiyo wahukohuko milele.
Wengi wanapata ajira wakishapata wanakimbilia mijini kwa kuwa huko ndipo walipo zaliwa, kwa gharama yoyote ile.
Zamani kila Halmashauri ilikuwa na malori kwa hiyo mtu anapewa barua ya uhamisho, jioni Lori la Halmashauri lipo nyumbani kwake linamuhamisha, akiwa na haki zake zote lakini siyo sasa watumishi wanakopwa.
Cha kusikitisha haya malori yapo lakini hayatengenezwi (yapo juu ya mawe).Mengi yakiwa na shida ndogondogo. Hata madereva wa halmashauri wapo wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi yoyote, muda mwingine wanaazimwa katika taasisi zingine, magari yote mabovu. Hakuna mpango wa kuyatengeneza hata kununua mapya, kama mpango wa kununua mapya upo basi ni ya magari ya viongozi tu.
Tengeneza malori, lipa watumishi, hamisha bila upendeleo wala kutazama majina ya mtoto wa fulani hakutakuwa na shida. Walimu watafundisha na miutasari ya masomo itakwisha na wanafunzi wetu watafaulu na likizo shule zitafungwa vizuri, vinginevyo tunadanganyana.
Malori haya ya kuwahamisha watumishi na magari mengine ya kuendeshea kazi za Halmashauri yalinunuliwa kwa wingi enzi za ujamaa hasa Uwaziri wa Chediel Mgonja, Jackson Makweta na Profesa Kigoma Malima sasa yanaoza.
Kwa sasa Watanzania wengi wanatambua umuhimu wa elimu kwa hiyo elimu ya saa za ziada haipingiki na tunapaswa kuiunga mkono kwa uvumba na ubani. Kwa leo naweka kalamu chini kwa chapuo la masomo ya ziada, nakutakia siku njema.
0717649257
Tags
Makala