NA MWANDISHI DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) imekuwa mshindi wa kwanza na kupata tuzo mbili za taasisi iliyoandaa vizuri taarifa za mahesabu kwa mwaka 2020.
Utoaji wa Tuzo za Umahiri katika Uandaaji wa Taarifa za Fedha ya Mwaka 2020 (Best Presented Financial Statements for the Year 2020 Awards) kwa taasisi, makampuni pamoja na mashirika zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) zilizofanyika katika Hoteli ya APC Bunju jijini Dar es Salaam Desemba 4, 2021.
Tuzo ya kwanza ni katika Kundi la Wizara na Idara zinazojitegemea (MDAs) za Kiserikali iliyoandaa vizuri Hesabu kwa Viwango vya Kimataifa kwa Sekta ya Umma (IPSAS) kwa mwaka huo na ya pili ni ya Mshindi wa jumla kwa MDAs zinazotumia IPSAS.
Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Gerald Musabila Kusaya wakati akipokea tuzo hizo, ameeleza kuwa, mbali na mamlaka kuweka mkazo katika kutekeleza majukumu yake ya udhibiti na mapambano dhidi ya dawa za kulevya bado imekuwa na umakini mkubwa katika kusimamia matumizi ya fedha.
Aidha, ameeleza kuwa, umakini huo ndiyo umeifanya mamlaka kuendelea kupata ushindi huo mfululizo ambao ni wa nne sasa.
Kuhusu mamlaka
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015.
Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa mamlaka kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.
Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.