Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Polisi washirikiana kuteketeza hekari 10 za mashamba ya mirungi

NA MWANDISHI MAALUM

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro,Desemba 10,2021 wamefanya operesheni maalum ya kuharibu mashamba ya mirungi zaidi ya hekari 10 katika Kitongoji cha Kindi, Kijiji cha Likweni, Kata ya Tae wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro. 

Katika operesheni hiyo inayoendelea, pia watu wawili wanashikiliwa kwa tuhuma za kusafirisha majani yanayodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya mirungi zaidi ya bunda 270.
Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Gerald Kusaya akishiriki kukata miti ya mirungi zaidi ya hekari 10 Desemba 10, 2021 katika mashamba ya mirungi Kitongoji cha Kindi kilichopo katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wakati wa Operesheni Maalum ya pamoja kati ya DCEA na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, kushoto kwake ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, ACP. Simon Marwa Maigwa.

Akizungumza wakati wa operesheni hiyo inayoendelea mkoani humo, Kiongozi wa Operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Bw. Gerald Kusaya amesema ni wakati sasa kwa; "Sehemu yoyote ile ambayo kutakuwa na dawa za kulevya, au mwananchi atakuwa anajihusisha na dawa hizo ikiwepo mirungi, au bangi au dawa nyingine yoyote inayopatikana mahali huko mitaani kwa maana ya Heroin, Cocaine na mengineyo ni wakati muafaka sasa akaachana na hii biashara haramu, maana hakuna hata siku moja ataweza kutushinda, tutamkamata tu,” amesema Kamishma Jenerali Kusaya.

Amesema, mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya udhibiti wamejipangakatika kuhakikisha wanapambana kwa kila namna katika kudhibiti biashara hiyo lengo likiwa ni kumaliza kabisa athari zitokanazo na matumizi ya dawa hizo

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Gerald Kusaya Desemba 10, 2021, akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya Operesheni Maalum ya pamoja ya kati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa kuharibu mashamba ya mirungi zaidi ya Hekari 10 katika Kitongoji cha Kindi kilichopo katika Wiaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

“Tunataka kuwa na Tanzania isiyokuwa na watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, tunashirikiana na vyema na Mamlaka nyingine za udhibiti , lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunamaliza kabisa matumizi ya dawa hizo nchini, ili mwisho wa siku tuwe na Tanzania isiyokuwa na dawa za kulevya na hii inawezekana, niwaombe watanzania wenye mapenzi mema na nchi yao kutoa taarifa kwa watu wanaojiuhusisha na biashara hii” amesisitiza Kamishna Jenerali Kusaya.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, ACP. Simon Marwa Maigwa amesema katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari mpaka Septemba mwaka 2020, jumla ya kesi 540 za dawa za kulevya ziliripotiwa mkoani humo na watuhumiwa 467.

Kamanda Maigwa amesema, katika kipindi hicho hicho kwa mwaka 2021 jumla ya kesi 678 ziliripotiwa huku watuhumiwa 561 ambapo kesi hizo zipo katika hatua mbalimbali mahakamani ikiwemo kwenye Mahakama ya uhujumu uchumi.

Aidha,amewaomba wananchi kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya dawa hizo ambazo zinaathiri nguvu kazi ya Taifa.
#KataaDawaZaKulevyaTimizaMalengoYako

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news