NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KANDARASI ya mwaka mmoja kati ya Kocha George Lwandamina na Azam FC imefutwa baada ya timu hiyo ya jijini Dar es Salaam kurekodi matokeo mabaya katika siku za karibuni.
Raia huyo wa Zambia amejiuzulu nafasi yake ya kuwanoa Wanalambalamba hao, ikiwa ni siku moja baada ya timu hiyo kulazimishwa sare ya 0-0 na Kagera Sugar.
Ni mtanange wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliopigwa katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.
George Lwandamina ambaye aliwahi pia kufundisha Yanga SC ya Dar es Salaam, ameiandikia barua Bodi ya Azam FC na kuishukuru kwa nafasi iliyompa katika klabu hiyo.
Katika barua yake, kocha huyo wa zamani wa ZESCO United ya Zambia amesema, amechukua uamuzi huo kwa maslahi ya klabu hiyo.
Uongozi wa Azam FC umeridhia hatua hiyo na moja kwa moja umemteua Mkurugenzi wa ufundi, Mmarekani mwenye asili ya Somalia, Abdihamid Moalin kukaimu nafasi hiyo hadi atakapotangazwa kocha mpya.
Lwandamina alijiunga na Azam FC mwezi Desemba mwaka jana kuchukua nafasi ya Mromania, Aristica Cioaba.
Ameiongoza Azam FC kwenye mechi rasmi 38 zikiwemo 30 za Ligi Kuu, nne za Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) na nne za Kombe la Shirikisho Afrika.
Azam mpaka sasa wanashika nafasi ya saba wakiwa na alama 11 baada ya kushinda mechi tatu, sare mbili na kupoteza mechi tatu.