NA LUCAS RAPHAEL
MKOA wa Tabora umepokea shehena ya tani 116 za mbegu za alizeti ikiwa ni mapokezi ya awali kati ya tani 240 ambazo ni kwa ajili ya msimu wa kilimo kwa mwaka 2021-2022.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt.Batilda Burian akimkabidhi mfuko wa mbegu za alizeti Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora, Seif Salum kwenye kituo cha Reli Tabora.
Alizeti hizo ni utekelezaji wa Mpango wa Serikali wa kukabiliana na tatizo la upungufu wa mafuta ya kula nchini ambao umeelekezwa kutatuliwa kupitia kilimo cha alizeti.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt.Batilda Burian alisema kwamba kufika kwa shehena hiyo ya mbegu za alizeti kutoka Wakala wa Mbegu nchini (ASA) itawasaidia wakulima mkoani humo.
Mkuu huyo wa mkoa wa Tabora alipokea shehena hiyo jana kwenye Kituo cha reli ya kati mkoani Tabora kutoka kwa Wakala wa Mbegu nchini (ASA).
RC huyo amekiri kufika kwa shehena hiyo ya mbegu za alizeti itasaidia kwenye kilimo kufikia lengo la kukabiliana na tatizo la upungufu wa mafuta ya kula nchini.
Hata hivyo aliwaagiza wakuu wa wilaya na Wakurugenzi kusimamia mbegu hizo ili ziweze kuleta tija.
Awali Afisa Masoko wa Wakala wa Mbegu nchini kutoka Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Luoga akizungumza kabla ya kukabidhi shehena hiyo alisema kwamba mkulima akilima mbegu hiyo ina uzao wa kumpatia magunia kati ya 7 hadi 11 zenye ujazo wa kilo 60 kwa ekari kulingana na huduma itakayotolewa wakati wa uzalishaji wake.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dkt.Batilda Burian akiwa ameshikilia mfuko wa mbegu za alizeti pembeni yake mkono wa kushoto aliyavaa suti ni Afisa Masoko wa ASA,Emmanuel Luoga na katika ni Katibu Msaidizi wa Huduma za Kilimo, Raphael Nyanda.
Aliendelea kusema kwamba wakulima walime mbegu hiyo kwa kufuata kanuni bora za kilimo na kuwahakikishia mavuno bora ambayo yataongeza upatikanaji wa mafuta mengi ya alizeti nchini.
Alisema kwamba wakala alipokea mahitaji ya mbegu za alizeti (Standard seeds) kwa mkoa wa Tabora zaidi ya tani 208 Kwa kuanzia ASA wamekabidhi tani 116 kati ya mahitaji yaliyoombwa.
Katika msimu huu wa 2021/22, Wakala wa Mbegu nchini ASA umepokea maelekezo ya Wizara juu ya maandalizi na usambazaji wa zaidi ya tani 2000 za mbegu ya alizeti zinazotarajiwa kuwafikia wakulima katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwahi msimu wa kilimo.
Serikali ilionesha maeneo ya kipaumbele katika halmashauri za mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara, Simiyu na Tabora.