Mbunge Dkt.Kaijage apiga tafu ujenzi jengo la Wajasiriamali UWT Kibaha Mjini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Dkt.Alice Kaijage amechangia kiasi cha 500,000 ujenzi wa jengo la wajasiriamali wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Kibaha Mjini.
Dkt.Kaijage aliunga mkono jitihada za ujenzi wa jengo hilo wakati wa sherehe za kuhitimisha sherehe za miaka 60 ya Uhuru ambapo UWT Kibaha Mjini waliadhimisha kwa kutembelea jengo hilo na kuangalia bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa umoja huo.

Amesema, ujenzi huo ambao unaendana na utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali ni kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kutaka wanawake kujikwamua kiuchumi.

"Kwa kuwapatia mafunzo wajasiriamali hawa ni jambo jema, kwani ukimkomboa mwanamke umeikomboa jamii na mnaungana na Rais kuipigania jamii ya Tanzania," amesema Dkt.Kaijage.
Aidha,amesema kuwa, wanawake ndiyo chachu ya maendeleo na moja ya kumuunga mkono Rais ni kufanya kazi kwa bidii na kuacha kuwa tegemezi.

Naye Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini, Eline Mgonja amesema kuwa, wanatoa mafunzo ya ujasiriamali bure ili kuwakomboa wanawake kiuchumi.

Mgonja ambaye ni mwalimu wa ujasiriamali na anawapatia mafunzo hayo wajasiriamali hao amesema kuwa, alipoingia madarakani kipaumbele chake ilikuwa ni kujenga sehemu kwa ajili ya wajasiriamali hao kuuzia bidhaa wanazozalisha.
Amesema kuwa,amewafundisha utengenezaji wa batiki, mafuta ya kula yanayotokana na mimea mbalimbali, sabuni za maji na bidhaa nyingine za kijasiriamali.

Naye mjasiriamali Rehema Sasia amesema kuwa,anashukiru UWT kwani sasa anauwezo wa kutengeneza vitu mbalimbali na kujipatia kipato ambapo mwanzo alikuwa hajui chochote.
Sasia amesema wamejifunza kutengeneza baadhi ya vitu ikiwemo Vicks ambayo huwa inatengenezwa nje ya nchi na wamejengewa uwezo wa kujitangaza na wanapata masoko nje ya mkoa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news