Mheshimiwa Mariam Ditopile amshukuru Rais Samia kwa maendeleo anayoyafanya Dodoma

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameendelea kuupa kipaumbele Mkoa wa Dodoma katika miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo Sekta ya Maji, Elimu na Miundombinu huku akiwaomba wananchi wa Kata ya Handali kumchagua Mgombea Udiwani wa kata hiyo, Emmanuel Madali.
Ditopile ametoa kauli hiyo wakati akimnadi Mgombea Udiwani wa Kata ya Handali wilayani Chamwino ambapo kata hiyo inafanya uchaguzi mdogo wa Udiwani kufuatia diwani aliyekuepo kujiuzulu nafasi hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi hao, Ditopile amesema Rais Samia ameyagusa maisha ya wananchi wa Dodoma ambapo katika sekta ya elimu ametoa kiasi cha Shilingi Bilioni 12 ambapo jumla ya Madarasa 601 yatajengwa bila wananchi kuchangishwa.

"Dodoma tuna bahati kubwa, Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametupatia fedha Shilingi Bilioni 12.02 ambazo zimeelekezwa katika kutatua changamoto ya madarasa mkoani kwetu ambapo madarasa 601 yatajengwa, lakini pia ametupatia Sh Bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa Shikizi 175 hii haijawahi kutokea.
"Kama hiyo haitoshi hapa Wilaya yetu ya Chamwino ambayo sisi Kata ya Handali tupo Rais Samia ametupatia jumla ya Sh Bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 64 lakini pia ameleta fedha kwa ajili ya Shule Shikizi 14, haya yote Rais Samia amefanya kwa mapenzi yake makubwa kwetu sisi wananchi wake," amesema Ditopile.
Amesema,katika Sekta ya Nishati, Rais Samia ameonesha kiu yake ya kumaliza changamoto ya umeme kwa wananchi ambapo katika kata hiyo ya Handali tayari vitongoji 15 kati ya 21 vimeshafikiwa na hivyo vilivyobaki ndani ya mwaka wa fedha wa 2021/22 vitakamilishwa.
"Rais wetu anataka kuona mkoa wetu wa Dodoma unapaa kimaendeleo, tayari ameidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 127 kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato ambapo pia Benki ya Maendeleo ya Afrika imetoa Dola Milioni 327 kukamilisha Uwanja huo utakaokua ukihudumia abiria Milioni 1.5 kwa mwaka. Kwetu hii ni fursa ya kukuza uchumi wa wananchi wote wa Dodoma,
"Kwahiyo ndugu zangu wa Handali naombeni mumchague Diwani Emmanuel Madali ili aweze kushirikiana na Mbunge wetu Lusinde na Rais Samia kusukuma maendeleo ya Kata yetu,"amesema Ditopile.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news