NA MWANDISHI DIRAMAKINI
KATIBU Tawala Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Dorothy Mwaluko leo Desemba 4, 2021 amefungua rasmi maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru Tanzania Bara yaliyofanyika kimkoa wilayani Manyoni mkoani Singida katika uwanja wa Jumbe ambapo watumishi mbalimbali walishirikishwa.
Kila mtu ana kipaji chake, vijana wakionyesha namna chakula kinavyoliwa katika mashindano.
Akihutubia mamia ya Watumishi kutoka wilaya ya Ikungi, Manyoni, Iramba, Singida Mjini, Mkalama na Itigi amewashukuru Watumishi hao kwa nidhamu kubwa walionesha wakati wa bonanza la michezo lililofanyika katika uwanja huo na kushirikisha michezo ya kuvuta kamba kwa wanawake na wanaume, netiboli, mpira wa miguu, kukimbiza kuku, mcho wa bao, riadha na mashindano ya kula.
Hata hivyo, RAS Mwaluko ametumia muda huo kuzipongeza timu mbalimbali zilizoshinda katika bonanza hilo pamoja na watumishi walioshiriki katika michezo na mazoezi mbalimbali ambapo aliwaasa kuendelea kufanya mazoezi hata baada ya bonanza kwisha ili kulinda afya zao.
Mheshimiwa Dorothy Mwaluko naye ameonyesha kipaji.
RAS Singida amewataka watumishi hao kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru kwa kujitathimini walipotoka walipo na wanapokwenda ili kuona maendeleo ambayo nchi yetu imeweza kuyafikia katika kipindi hicho.
Dorothy Mwaluko akaenedelea kufafanua kwamba Mkoa wa Singida una fursa nyingi ikiwemo za kitalii ambazo zikitumika vizuri zitaongeza vipato vya wananchi na kuboresha maisha yao.
Aidha, akawataka watumishi hao kuadhimisha miaka 60 kwa kujitathmini namna wanavyoutumia muda wao kwa kutambua kwamba ni mtaji ambao kama hautatumika vizuri mafanikio hayataweza kufikiwa.
Kwa upande wake Henry Kapera Afisa michezo wa Mkoa wa Singida akimkaribisha mgeni rasmi ambaye ni RAS Singida amesema, lengo la michezo hiyo ni kuadhimisha miaka 60 ya uhuru na kuwajenga watumishi kiafya.
Hata hivyo Kapera aliwaomba wananchi wa Mkoa huo wanawake na wanaume kujitokeza na kushiriki michezo mbalimbali inayoendelea uwanjani hapo kama sehemu ya mazoezi, lakini kuonesha vipaji vyao.
Aidha, Kapera alibainisha kwamba baadhi ya timu zilichelewa kufika uwanjani hapo kutokana na sababu mbalimbali hivyo wangeweza kuendelea na michezo mbalimbali baada ya mgeni rasmi kuondoka.
Kapera akamalizia kwa kusema mkoa una mkakati kabambe kuendeleza michezo hiyo pamoja na kufanya mazoezi ya mara kwa mara.