Mkurugenzi wa HGWT,Rhobi Samwelly akabidhi tuzo kwa IGP Sirro,maafisa 18 wa polisi katika kuwezesha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili nchini

NA FRESHA KINASA

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia lenye makao makuu yake Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amekabidhi tuzo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly (kulia) katikati ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Khamis Hamza Chillo wakimkabidhi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng'anzi tuzo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini,IGP Sirro. (Picha zote na DIRAMAKINI BLOG).
Afisa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto, Annastazia Hipolite Olomi akipokea tuzo
Sambamba na maafisa na askari 18 wanaofanya kazi Dawati la Jinsia na Watoto mikoa mbalimbali nchini katika kutambua na kuthamini juhudi zao katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Rhobi amekabidhi tuzo hizo leo Desemba 10, 2021 katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa, Wakaguzi na askari wanaofanya kazi Dawati la Jinsia na Watoto unaofanyika kwa siku mbili Katika Shule ya Sekondari Mwanza iliyopo jijini Mwanza na kuhudhuriwa na viongozi wa polisi, Serikali, mashirika pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Khamis Hamza Chillo ambapo unalenga kufanya tathimini ya mambo mbalimbali katika kuimarisha ufanisi na utendaji wa kazi wa dawati hilo.
Afisa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti Sijali Nyambuche akipokea tuzo kutoka kwa Mkurugenzi wa HGWT Rhobi Samwelly katikati ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mh. Khamis Hamza Chillo.

Rhobi amesema kuwa, kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Sirro katika mapambano ya Ukatili wa Kijinsia pamoja na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Dawati la Jinsia kutoka mikoa mbalimbali nchini ameamua kutoa tuzo hizo ili kuthamini juhudi zao sambamba na kuwatia moyo na kuwapa hamasa zaidi ya kufanya kazi.
"Kwa Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara, Sijali Nyambuche na Annastazia Hipolite Olomi hawa ni maafisa wa Dawati la Jinsia na Watoto wamekuwa wakifanya kazi kwa kujituma muda wote, iwe usiku ama mchana kunapotokea kuna watu wanataka kufanya vitendo vya ukatili lazima wachukue hatua mara moja na pia wamekuwa wakishughulikia matukio ya ukatili wa kijinsia kwa weledi ikiwemo kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji," amesema Rhobi.

"Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania pamoja na wadau wengine tumeendelea kufanya nao kazi kwa karibu sana katika Wilaya ya Serengeti, nimeamua kutoa tuzo kwa maafisa hawa na wengine ambao majina yao nilipewa kutokana na ufanisi wao bora wa kazi kutoka mikoa mingine akiwemo IGP Sirro ambaye yuko mstari wa mbele kuhakikisha ukatili hauna nafasi katika jamii, kwani katika ziara zake mbalimbali amekuwa akikemea vitendo hivyo na kusisitiza elimu itolewe kwa wananchi,"amesema Rhobi.
Aidha, Rhobi amewashukuru Maafisa, Wakaguzi na askari wote wanaofanya kazi Dawati la Jinsia na Watoto kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika kuhakikisha ukatili unaisha, ambapo pia amesema mshikamano thabiti baina ya Serikali, wadau na wananchi unahitajika kumaliza ukatili wa kijinsia akasisitiza kila mmoja kushiriki katika jambo hilo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chillo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kutoa ushahidi mahakamani pindi watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani badala ya kumaliza kesi hizo kwa njia ya mazunguzo ya kifamilia hatua ambayo inafifisha juhudi za serikali na wadau mbalimbali kutokomeza vitendo hivyo huku pia akiomba elimu ya madhara ya ukatili izidi kutolewa kwa wananchi.
Pia Naibu Waziri huyo amesema, Serikali haitawafumbia macho askari polisi, madaktari ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa wakiharibu ushahidi unaowezesha kuwatia hatiani watuhumiwa wakati wanafanya uchunguzi na hivyo watuhumiwa kuachiwa huru

"Kila mmoja atimize wajibu wake, kama ni daktari umeletewa mtu aliyefanyiwa ukatili ufanye uchunguzi tenda haki, Kama ni polisi unafanya uchunguzi wa kesi tenda haki usishiriki kutetea mhalifu tukibaini mtumishi wa Serikali uko sehemu ya kurudisha nyuma juhudi za serikali kumaliza ukatili hakika tutashughulika na wewe. Wazazi pia wafuatilie Maendeleo ya watoto wao kujua Kama wako salama muda wote," amesema Naibu Waziri.
Kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazolikabili Dawati la Jinsia na Watoto ikiwemo upungufu wa ofisi, magari ya usafiri, vifaa vya ofisi na mambo mengine, Naibu Waziri amesema changamoto hizo amezichukua kwa ajili ya kutafuta namna ya kuzipatia ufumbuzi ambapo pia ameomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kujitolea kusaidia kuzitatua katika maeneo yao.
Sijali Nyambuche ni Afisa wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Serengeti ambapo ameshukuru kupokea tuzo hiyo, na ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi katika kupambana na vitendo vya ukatili ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi wa Serengeti.

Faidha Yusuph Suleiman ni Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Makao Makuu ambapo amesema, dawati hilo limeendelea na majukumu mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia na kwamba wananchi wameendelea kupata uelewa mpana sambamba na kuwa na mfumo wa kurekodi matukio mbalimbali ya ukatili wa kijinsia.

Ameongeza kuwa, dawati hilo linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa magari maalumu ya kufanyia kazi hasa kwenda vijijini, vifaa vya ofisi na baadhi ya maeneo kutokuwa na ofisi maalumu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news