NA ANGELA MSIMBIRA-OR TAMISEMI
DOKTA Stephen Kibusi wa Shule Kuu ya Uuguzi na Afya ya Jamii Chuo Kikuu cha Dodoma amesema waratibu wa afya ngazi ya mikoa ni muhimili katika kuleta mabadiliko kwenye afua za afya, hivyo wana wajibu wa kusimamia suala zima la uimarishaji wa afya kwa jamii.
Akifungua mafunzo ya siku tano ya uimarishaji afya kwa waratibu wa Afya Mikoa Dkt.Kibusi amesema, kuwawezesha waratibu wa Afya wa Mkoa kutasaidia kuleta mabadiliko chanya kwa jamii na kutasaidia afua za afya kujulikana na kutekelezwa kwa mujibu wa sera na miongozo ya Serikali.
Amesema kuwa, jamii ikielewa umuhimu wa uimarishaji wa afya itasaidia kupunguza magonjwa ambayo yamekuwa ni kikwazo katika maendeleo nchini kwa kuwa jamii yenye afya duni hushindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu kutokana na maradhi.
Dkt. Kibusi amesema, uwepo wa mifumo mizuri kuanzia ngazi ya watunga sera hadi watekelezaji kutasaidia suala zima la uimarishaji wa afya nchini na kuwa taifa imara lenye jamii yenye afya bora ambao wanaweza kutekeleza majukumu yao kimilifu na kuleta maendeleo kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla.
Aidha, amesema maudhui ya mafunzo hayo yatasaidia kuziwezesha timu za Mikoa kuwa na nguvu ya kusimamia na kuratibu suala zima la uimarishaji afya nchini, hii itasaidia katika kupambana na magonjwa ya mlipuko yanayojitokeza nchini.
Ameendelea kusema kuwa, magonjwa yasiyoambukizwa yamekuwa ni changamoto nyingine ambayo inahitaji kuwekewa mkazo kwenye suala zima la utoaji wa elimu ya kutosha kwa jamii ili kujenga jamii kujitambua, kudhibiti magonjwa yanayotokana na ulaji na mtindo wa maisha.
“Tunahitaji kuwa na makakati wa timu za Waratibu wa Mkoa ambazo zitasaidia katika kulitekeleza jambo hilo,"amesema.
Naye Mratibu wa Afya Jamii Kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Martha Mariki amesema kuwa, Serikali ina wajibu wa kuwekeza katika suala zima la afya ya jamii kwa kuwa asilimia kubwa magonjwa yanasumbua sana katika sekta ya afya kwa kuwa afya ya jamii haijakaa katika nafasi yake.
“Kama waratibu wa afya ya jamii hawajakaa katika nafasi yao vizuri tutegemee magonjwa mengi ya mlipuko na magonjwa mengine yanayoweza kuzuilika, hivyo wanawajibu wa kusimama katika nafasi zao ili afya za jamii ziweze kuimarika na kujenga jamii yenye afya bora katika Sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa,”amesema.
Awali, Meneja Mradi wa HPSS-Tuimerishe Afya, Ally Kebby amesema, pamoja na kufadhili mafunzo hayo, pia wametoa vifaa mbalimbali va kujifundishia na kujifunzia kwa Chuo Kikuu cha Dodoma vyenye thamani ya Sh milioni 21.
Amesema, vifaa hivyo vitasaidia kuboesha kuboresha kazi ya kutoa mafunzo ya afya na utafiti ili kusaidia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinisa, Wazee na watoto pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na wadau wengine katika mipango ya kuimarisha afya.