NA MWANDISHI DIRAMAKINI
SHIRIKA la Mazingira la WildAid lenye makao yake makuu San Francisco jijini California, Marekani limemtangaza mwimbaji Nakaaya Sumari kuwa miongoni mwa mabalozi wake wa heshima.
Sumari anaungana na mastaa wengine kama Ben Pol, Mohammed Dewji, Anne Kansiime, Sauti Sol, Eliud Kipchoge, David Beckham, Lupita Nyong'o na Leonardo Dicaprio.
"WildAid inalenga kupunguza mahitaji ya bidhaa za wanyamapori, inafuraha kutangaza kusainiwa kwa Balozi mpya wa Tanzania, Nakaaya Sumari (The Lioness) ambaye anaungana nasi kwa shauku kuunga mkono kampeni yetu ya Simba, anaungana na wengine kama Antu Mandoza, Benjamin Fernandes na Fahad Fuad kuwatetea simba,"wameeleza.
Naakaya ambaye ana Stashahada ya Usimamizi wa Wanyamapori na Waongoza Watalii na uzoefu mkubwa wa kazi katika sekta ya utalii anaamini kuwa, Tanzania ina urithi wa asili tofauti na wa kipekee ambao unahitaji kulindwa.
“Ni miaka mingi nimefanya kazi za kitalii na uhifadhi, kwa mara ya kwanza nimeonekana na kutambulika na WildAidAfrica, ni heshima na furaha kubwa sana, napenda sana wanyama hasa simba jike,"amesema Nakaaya.
WildAid limekuwa mstari wa mbele kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali katika kuunga mkono juhudi za kukomesha biashara haramu ya wanyama pori.
Sambamba na kupungiza mahitaji ya bidhaa zitokanazo na wanyama hao kupitia kampeni za uhamasishaji zinazofanyika mara kwa mara.
Kampeni zao huwa zina lengo la kukuza uelewa kwa wananchi kuhusu kukithiri kwa uwindaji haramu na kuongeza jitihada za kuwalinda tembo, Simba na wanyama wengine wa porini.