NA GODFREY NNKO
MOYO wa upendo, ukarimu kwa rika, kabila na itikadi zote,mshikamano na umoja ndiyo vinamfanya Nabii Mkuu Tanzania, Dkt.Geordavie kuwa kati ya viongozi bora zaidi ndani na nje ya Tanzania.
Hivi karibuni, Dkt.Geordavie ameendelea kugusa maisha ya wengi akiwemo Goodluck Gozbert ambaye amemzawadia gari jipya aina ya Mercedes Benz.
Gozbert ambaye ni mzaliwa wa jijini Mwanza ambapo kwa sasa anaishi jijini Dar es Salaam ni mwimbaji wa nyimbo za injili kutoka Tanzania. Goodluck anajulikana kwa sauti yake nyororo.
Tangu utotoni mwake, Goodluck Gozbert alikuwa na hamu ya kuimba na kufanya mziki. Katika mahojiano ya hapo awali, Gozbert alisema kuwa hakuwa na nia ya kufuata muziki kama taaluma, lakini kwa sababu ya ugumu wa maisha alilazimika kukuza talanta yake.
Miongoni mwa nyimbo maarufu za Goodluck Gozbert ni Simu, Hasara Roho,
Umeshinda Yesu,Kama si yeye,Ipo siku,
Shukrani Nibaliishe,Mama,Mwenye Majibu,
Pendo Langu,Shukurani na nyingine nyingi.
Katika kipindi chake katika muziki,Gozbert aliteuliwa na kushinda tuzo kadhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mwaka 2019, alipokea mataji tano wakati wa Tuzo za Maranatha Afrika Mashariki ambazo zinaheshimu matendo bora ya injili kutoka Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea, na Somalia.
Mnamo mwaka wa 2015, Goodluck Gozbert alishinda Msanii wa Kiume wa Mwaka wa Afrika Mashariki kwenye Tuzo za Sauti, na Msanii Bora wa Injili / Wimbo wa Mwaka kwenye Tuzo za Xtreem. Katika mwaka huo huo, alishinda pia Msanii Bora wa Nyimbo za Injili Tanzania / Wimbo wa Mwaka kwenye Tuzo la Xtreem.
Mbele ya umati mkubwa wa watu chini ya Nabii Mkuu Tanzania, Dkt.Geordavie katika huduma yake ya GeorDavie Ministries Int'l (GDMi) iliyopo Kisongo jijini Arusha, mwimbaji huyo alikabidhiwa gari hilo na fedha taslimu Shilingi Milioni 2 kwa ajili ya mafuta na magurudumu.
Hafla hiyo ilikuwa ni mwendelezo wa dhifa za Kifalme zinazofanyika katika mji wa Daudi chini ya Dkt.Geordavie.
Dkt.GeorDavie ni mtumishi wa Mungu, ambaye ameendelea kutumika katika huduma kwa miaka 40 iliyopita.
Ni Rais mwanzilishi na Askofu Mkuu wa kanisa hilo kubwa la Kinabii linalokuwa kwa kasi jijini Arusha, Tanzania na lenye waumini kote Afrika, Ulaya, Marekani na mabara mengine.
Mungu alianza kumtumia GeorDavie tangu akiwa mtoto mdogo. Wazazi wake walimshuhudia akitabiri akiwa na umri wa miaka mitano kwa usahihi sana na mambo yalitokea kadri ya utabiri wake.
Mwishoni mwa miaka ya 70, Mungu alimwita rasmi katika utumishi wa Ufalme kupitia huduma mbalimbali, kuanzia kuongoza sifa na kuabudu, hadi kuwa Mmisionari wa Kitume, Mwalimu wa Biblia, Mwinjilisti, Mchungaji, pamoja na kuanzisha Global Concert Ministries ambapo aliwaongoza vijana katika kukuza vipaji vyao.
Baadaye alianzisha Kituo cha Lighthouse kwa watoto wa mitaani ambapo aliweza kushughulikia changamoto zao na kutoa mwanga katika jamii kwa watoto wa mitaani katika Ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania kwa kuwapatia chakula, nguo, malazi na elimu.